UTPC KUTAFUTA FEDHA KUSOMESHA WANACHAMA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI


Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania(UTPC), Abubakar Karsan
******
MKURUGENZI Mtendaji wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania(UTPC), Abubakar Karsan  amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau itatafuta fedha za kugharimia wanachama wa klabu wasiokuwa na Shahada ili wakidhi matakwa ya Sheria ya Huduma ya Kupata Habari inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi karibuni endapo serikali itakubali kuongeza muda wa kuanza kutumika.

Alitoa msimamo huo wa UTPC wakati akichangia hoja katika ajenda iliyotoa maelezo kuhusu Muswada wa Sheria ya Kupata Habari iliyowasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile kwenye mkutano mkuu wa wanachama wa UTPC uliomalizika juzi jijini Mwanza.

Kauli ya Mkurugenzi huyo imetokana na uwepo wa moja ya vipengele vilivyomo ndani ya muswada huo hasa kile kinachoeleza utaratibu wa kumtambua mwandishi wa habari ambaye atalazimika kuwa na elimu ya kiwango cha Shahada katika Uandishi wa Habari, Mawasiliano ya Umma au taaluma nyingine ili kumuwezesha kufanya ‘specialization’ katika sekta mbalimbali kipengele ambacho kimsingi kinadaiwa kwamba kinagusa idadi kubwa ya waandishi wa habari.

Alisema kwa sababu UTPC ni asasi mwamvuli ya klabu za waandishi wa habari wa mikoa yote hapa nchini siku zote itaendelea kuunga mkono jambo lolote linalogusa uhai na maslahi ya waandishi ambao ni wanachama hai ndani ya klabu ikiwemo kuwaendeleza kitaaluma ili waendane na mabadiliko yanayotokea.

"Ili kufanikisha mchakato huo wa kukusanya maoni napenda kuwahakikishia kwamba UTPC itaratibu shughuli hiyo ya utoaji maoni kuhusu muswada huo ndani ya klabu mikoani ili kutoka na kauli moja," alisema.

Karsan alisema ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa hivi sasa klabu katika kila mkoa zinaendelea kukusanya taarifa sahihi kuhusu wasifu wa kila mwanachama wake ili kupata takwimu sahihi zitakazojazwa kwenye daftari maalumu ambazo zitatoa idadi na mahitaji halisi ya wanaohitaji kuendelezwa kitaaluma.

Imeandikwa na Anna Makange, Mwanza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527