Na OWM – TAMISEMI, Bagamoyo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha wanawasimamia Wakurugezi wa Halmashauri wakati wanapoandaa bajeti za Mwaka wa Fedha 2026/27 kuweka vifungu vya kugharamia maboresho ya miundombinu ya elimu, ili kujiaanda na mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028 ambapo kwa mujibu wa mtaala mpya watapokelewa wanafunzi waliohitimu darasa la sita na la saba.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo, akiwa katika kikao kazi cha kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Halmashauri ya Mji Bagamoyo, mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya mendeleo katika halmashauri hiyo ya mji.
“Mwaka 2028 kutokana na mtaala mpya watakaohitimu darasa la sita na la saba watajiunga na kidato cha kwanza, hivyo yatengwe mafungu kwenye bajeti mtakazoandaa ili kusiwe na maandalizi ya zimamoto tunapojianda kupokea wanafunzi hao,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuhakikisha wanapata makadirio sahihi ya idadi ya wanafunzi watakaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028, ili bajeti zitakazotengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu zikidhi mahitaji.
Akiwa katika ukaguzi wa miundombinu ya Shule ya Sekondari Shishila Lwada iliyopo kata ya Mapinga Bagamoyo, Prof. Shemdoe ameelekeza ujenzi wa madarasa matatu katika shule hiyo ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na mapokezi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028.
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, Mdau wa Maendeleo Bw. Gaston Francis amejitolea kujenga madarasa mawili yenye thamani ya Shilingi Milioni 50 katika Shule hiyo ya Sekondari Shishila Lwada na kufanya idadi ya madarasa mapya yatakayojengwa kufikia matano (5).
Prof. Shemdoe amemshukuru mdau huyo wa maendeleo kwa kuiunga mkono Serikali katika maboresho ya miundombinu ya elimu.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa Kidato cha Nne wa Shule hiyo Bi. Disisheni Mwasele amemshukuru Prof. Shemdoe kwa maelekezo aliyoyatoa kwakuwa yatasaidia kupunguza changamoto ya uchache wa madarasa na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Naye, Kaka Mkuu wa Shule hiyo Bw. Yusuph Anderson Joseph
amesema kuwa, anashukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuboresha miundombinu katika shule hiyo, kwakuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la wanafunzi ambao idadi yao inafikia 1600.
Prof. Shemdoe akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Bagamoyo, amekagua mradi wa ujenzi wa vyumba viwili (2) vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Shushila Lwada, Ujenzi wa Jengo la Utawala, Ujenzi wa Mabweni mawili (2), bwalo na vyumba viwili (2) vya madarasa katika Shule ya Sekondari Matimbwa, ujenzi wa jengo la watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, matumizi bora ya nistati katika soko la samaki pamoja na kufanya kikao kazi na watumishi.










Social Plugin