Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAANDISHI WAHIMIZWA KUTOA ELIMU KUHUSU DAWA ZA KULEVYA


Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imebainisha kuwa mwaka 2025 ilikamata tani 31.76 na lita 183,500 za kemikali bashirifu, huku ikizuia tani 734 kuingia nchini kinyume cha sheria, ikisema waandishi wa habari wanapaswa kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya uhalifu huo kupitia utoaji wa taarifa sahihi kwa umma.

Hayo yameelezwa leo Julai 3, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya.

Mafunzo hayo yalihusisha mada kuhusu dawa tiba zenye asili ya kulevya, dawa mpya za kulevya, maabara bubu za kutengeneza dawa za kulevya, madhara ya matumizi ya dawa hizo pamoja na udhibiti wa kemikali bashirifu zinazotumika katika uzalishaji wa dawa haramu.

Akitoa mada kuhusu kemikali bashirifu na sheria zinazozisimamia, Kamishna Msaidizi wa Uchunguzi wa DCEA, Ziliwa Machibya, alisema udhibiti wa kemikali hizo unasimamiwa na Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani (Udhibiti na Usimamizi) Na. 3 ya mwaka 2003, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 (Toleo la 2020), hususan vifungu vya 14, 15 na 15A, pamoja na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Na. 1 ya mwaka 2003 iliyofanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2019.

Aliongeza kuwa Tanzania pia inatekeleza Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1988 wa Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya na Kemikali Bashirifu, ambao unaweka misingi ya usimamizi wa kemikali zinazoweza kutumika kuzalisha dawa za kulevya.

Machibya alisema kemikali bashirifu zinazokamatwa katika operesheni mbalimbali duniani ni pamoja na acetone, ethanol, hydrochloric acid, lead acetate, methylamine, benzyl alcohol, toluene, tartaric acid na nyinginezo ambazo hutumika katika utengenezaji wa dawa mbalimbali za kulevya.

Akitoa mifano ya matukio yaliyobainika nchini, alisema uchunguzi uliwahi kubaini kilo 12 za kemikali aina ya pseudoephedrine zilizochepushwa wakati wa uzalishaji wa dawa za kikohozi, hali iliyosababisha kuharibiwa kwa lita 10,000 za dawa zilizokuwa na kiwango pungufu cha kiambata hicho.

Aidha, alisema mamlaka hiyo ilifuatilia na kubaini usafirishaji wa tani 21.7 za kemikali aina ya acetic anhydride kutoka Tanzania kwenda nchini Pakistani kwa kutumia jina bandia la acetic acid, tukio lililodhihirisha mbinu mpya zinazotumiwa na mitandao ya biashara haramu ya dawa za kulevya.

Machibya alisema mafanikio ya operesheni zilizofanyika mwaka 2025 yaliwezesha kukamatwa kwa tani 31.76 na lita 183,500 za kemikali bashirifu nchini, huku tani 734 zikizuiwa kuingia nchini kinyume cha taratibu zilizowekwa.

Alifafanua kuwa kiasi hicho kilijumuisha tani nne za kemikali zilizokuwa zitumike kutengeneza dawa ya kulevya aina ya fentanyl ambazo zilikuwa zimepangwa kusafirishwa kwenda Mexico kwa kutumia jina bandia la protein biotine.

Vilevile, alisema uchunguzi uliwezesha kubaini maabara bubu ya kutengeneza dawa ya kulevya aina ya methamphetamine katika eneo la Namanga, upande wa Kenya, hatua iliyoonyesha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kudhibiti biashara hiyo.

Aliwataka waandishi wa habari kutumia mafunzo hayo kuandika habari zenye kuelimisha umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya, mbinu zinazotumiwa na wahalifu pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria katika udhibiti wa kemikali bashirifu, akisisitiza kuwa vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com