Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SAJENTI NOELA AIPEPERUSHA VYEMA BENDERA YA TANZANIA KATIKA MISHENI YA UNMISS


Sajenti wa Polisi (SGT) Noela Pallangyo kutoka Jeshi la Polisi Tanzania anayeitumikia Misheni ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS), ametunukiwa barua ya pongezi kutokana na utendaji wake uliotukuka, weledi, na mchango mkubwa alioutoa katika utekelezaji wa majukumu ya kulinda amani katika taifa hilo.


Katika kutambua huduma yake ya mfano, Umoja wa Mataifa umemsifu SGT Noela kwa bidii, umahiri, na weledi wake wa hali ya juu alipokuwa akitekeleza majukumu yake kama Afisa wa Rasilimali Watu (Personnel Officer) katika Makao Makuu ya Misheni hiyo (MHQ).


Tathmini ya UNMISS inaeleza kuwa mchango wake umekuwa na tija kubwa kwa misheni hiyo, ikisaidia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa wajibu wa msingi wa kulinda amani nchini humo.


Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, SGT Noela alionyesha unyenyekevu kwa kueleza kuwa heshima hiyo si ya kwake binafsi bali ni ushindi kwa taifa la Tanzania na Jeshi la Polisi kwa ujumla. Aidha, hakusita kuonyesha shukrani zake za dhati kwa viongozi wake pamoja na askari wenzake, akisisitiza kuwa ushirikiano mkubwa aliopewa na timu yake ndio uliomwezesha kufikia mafanikio hayo makubwa katika jukwaa la kimataifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com