Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akiwa pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Edward Ngelela (kulia), wakikagua moja ya vituo vya waendesha bodaboda vilivyozinduliwa katika Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Vituo hivyo vimetengenezwa na Mhe. Azza Hillal Hamad kwa ajili ya kuwawezesha waendesha bodaboda kufanya shughuli zao katika mazingira rasmi na yenye utaratibu.

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akizungumza leo Julai 18, 2026 wakati wa uzinduzi wa vituo vitatu vya waendesha bodaboda alivyovijenga katika Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kwa lengo la kuwawezesha waendesha bodaboda kufanya shughuli zao katika mazingira salama na yenye utaratibu.

Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa vituo vya waendesha bodaboda alivyovijenga katika Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kufanya shughuli zao katika mazingira rasmi na salama.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mhe. Azza Hillal Hamad, amewataka wananchi, hususan waendesha bodaboda, kuendelea kuilinda amani ya Tanzania, akisisitiza kuwa Watanzania hawana sehemu nyingine ya kukimbilia zaidi ya Mama Tanzania, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama, yenye umoja na utulivu.
Mhe. Azza ametoa wito huo leo Julai 18, 2026 wakati akizindua rasmi vituo vitatu vya waendesha bodaboda alivyovijenga katika Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha vijana kufanya shughuli zao katika mazingira rasmi na yenye utaratibu, ambapo amewahimiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutokubali kushawishiwa na mtu yeyote kuvuruga amani iliyopo.
"Asitokee mtu yeyote aje kuwadanganya mkavunja amani mliyonayo. Tukaeni kwa amani, tuipende nchi yetu, tupende familia zetu na tuwaheshimu wazazi wetu. Kazi hii tunayofanya ya kutafuta riziki inatokana na amani tuliyonayo, si vinginevyo," amesema.
Mbunge huyo amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo ya wananchi na kwamba bila utulivu shughuli za kiuchumi haziwezi kustawi, ikiwemo shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo zinazofanywa na waendesha bodaboda kila siku.
Amesema wananchi wa Itwangi wanapaswa kujifunza kutokana na hali inayojitokeza katika baadhi ya maeneo na kuhakikisha jimbo hilo linaendelea kuwa mfano wa mshikamano, upendo na utulivu.
"Tunajionea maeneo mengine, lakini hatutaki Jimbo la Itwangi likose amani. Hatuna sehemu nyingine ya kukimbilia zaidi ya Mama Tanzania. Hatuna sehemu nyingine ya kukimbilia zaidi ya Shinyanga. Naomba tuendelee kuitunza amani tuliyonayo, tuishi kwa amani na tuishi kwa upendo",amesema Azza.
Mhe. Azza amewataka vijana kutanguliza uzalendo na kutumia nguvu zao kujitafutia kipato halali badala ya kukubali kushawishiwa kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii na maendeleo ya Taifa.
"Asije mtu kuwashawishi kwa jambo lolote. Twendeni tukafanye kazi zetu kwa amani. Tukilinda amani, tutalinda pia ajira zetu, familia zetu na maendeleo ya watoto wetu," amesisitiza.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, hivyo ni muhimu wananchi waendelee kuitunza amani inayowezesha utekelezaji wa miradi hiyo na kukuza uchumi wa Taifa.
Mbunge huyo amewahimiza waendesha bodaboda kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao kwa kuelimishana, kuheshimu sheria za nchi na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudumisha utulivu.
Uzinduzi wa vituo hivyo vya waendesha bodaboda ni sehemu ya juhudi za Mbunge huyo za kuwawezesha vijana kufanya shughuli zao katika mazingira yaliyo rasmi, salama na yenye utaratibu, ili kuongeza fursa za kujipatia kipato na kuboresha maisha yao.
Mhe. Azza amesisitiza kuwa mafanikio ya juhudi hizo yanategemea uwepo wa amani, akiwataka waendesha bodaboda na wananchi kwa ujumla kuendelea kuilinda na kuithamini amani iliyopo, ambayo imeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya Jimbo la Itwangi na Taifa kwa ujumla.
Mara baada ya uzinduzi wa vituo hivyo vya waendesha bodaboda, Mhe. Azza Hillal Hamad ameendelea na shughuli nyingine ya kukabidhi gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya Kituo cha Afya Tinde, gari lililotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Jimbo la Itwangi.
Baada ya makabidhiano hayo, viongozi wa mila wa Tinde walimkabidhi Mhe. Azza zawadi ya vazi la kimila pamoja na fimbo ya heshima, huku wakimtunuku jina la kimila "Balele", lenye maana ya "Mlezi", ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuwatumikia wananchi na kusimamia masuala ya maendeleo katika Jimbo la Itwangi.




















Social Plugin