Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amewahakikishia Watanzania kuwa nchi ipo salama na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo bila hofu yoyote.

Akitoa kauli hiyo jijini Dodoma leo, Julai 17, 2026, wakati wa ziara ya ukaguzi wa maandalizi ya Siku ya Mashujaa inayotarajiwa kufanyika Julai 25, 2026, katika Viwanja vya Mashujaa, Mtumba, Waziri Katambi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake thabiti ambayo yameendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa taifa.

Waziri Katambi amesisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kudhibiti vitisho vyovyote vya nje huku vikiongeza nguvu katika kuimarisha ulinzi wa mipaka na kuhakikisha usalama wa ndani ya nchi unabaki kuwa kipaumbele cha juu.


Katika kusisitiza utulivu huo, Waziri Katambi amebainisha kuwa wote wako salama, wakiwemo wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wageni wote wanaoingia nchini kwa kufuata taratibu zilizowekwa. Ziara hiyo ya ukaguzi iliongozwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ambaye alipokea taarifa ya maandalizi ya kilele cha maadhimisho hayo ya kitaifa.