Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Savera Salvatory, ameielekeza Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kuongeza juhudi katika kutangaza huduma zake zinazotolewa kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ili kuwafikia waandishi wengi zaidi na kuwahamasisha kupata huduma kwa wakati.
Bi. Savera amesema hatua hiyo pia itasaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu ya JAB pamoja na umuhimu wa waandishi wa habari kuwa na ithibati kwa mujibu wa sheria na miongozo inayosimamia taaluma hiyo.
Ameyasema hayo leo, Julai 4, 2026, alipofanya ziara katika Kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kinachoshirikisha taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara hiyo, ambapo alijionea huduma na elimu inayotolewa kwa wananchi na wadau wanaotembelea maonesho hayo.
Katika ziara hiyo, Bi. Savera alipata fursa ya kutembelea banda la JAB na kujionea namna huduma za ithibati, usajili pamoja na utoaji wa elimu kuhusu taaluma ya uandishi wa habari zinavyotolewa kwa waandishi na wananchi.
Aidha, aliambatana na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Bi. Zahra Guga, ambaye alimpongeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, kwa usimamizi wake wa karibu wa shughuli za banda hilo kupitia ziara za mara kwa mara wakati wa maonesho.
Bi. Guga alisema uwepo wa viongozi katika banda la JAB unachochea uwajibikaji, huongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuimarisha utoaji wa elimu kwa wadau wanaotembelea maonesho ya Sabasaba.


Social Plugin