Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JWTZ YATOA TAHADHARI DHIDI YA VURUGU, YASISITIZA HATUA ZA KISHERIA KWA WATAKAOVUNJA AMANI



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa tahadhari kwa wananchi dhidi ya kushiriki au kuhamasishwa kushiriki katika vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani, likisisitiza kuwa litachukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayejihusisha na vitendo vinavyohatarisha usalama wa nchi.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Julai 4, 2026 na Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Sylvester Mangure, Jeshi limesema hali ya mipaka ya Tanzania na usalama wa ndani ya nchi ni shwari kutokana na ushirikiano uliopo kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda amani na utulivu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mazingira ya amani yaliyopo yamewawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji na maendeleo, huku ikibainisha kuwa kuna watu wanaoendelea kutumia njia za uchochezi na upotoshaji kuwashawishi wananchi kushiriki katika vitendo vya vurugu vinavyolenga kuvuruga utulivu wa nchi.

JWTZ limeonya kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo kuhatarisha maisha ya wananchi, kuharibu mali, kusimamisha shughuli za uzalishaji na kudhoofisha uchumi wa Taifa.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi limewataka wananchi kupuuza wito wowote unaohamasisha vurugu na kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu, huku likisisitiza kuwa lina mamlaka ya kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Ulinzi wa Taifa dhidi ya wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Aidha, JWTZ limewahimiza wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji, mitaa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu viashiria vyovyote vya uchochezi au uvunjifu wa amani ili hatua zichukuliwe mapema.

Jeshi pia limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda nchi, Katiba na wananchi, pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha amani, utulivu na umoja vinaendelea kudumishwa kwa maslahi ya Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com