Na mwandishi wetu,Mwanza
Mameneja wa TARURA wa Mikoa nchini wametakiwa kuwa na jukwaa moja na mpango kazi na Wakufunzi wasaidizi ili waongee lugha moja katika kufanikisha Mpango wa Matengenezo ya Barabara kwa Kutumia Vikundi vya Kijamii (CBRM).
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Edward Amboka wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Mameneja wa Mikoa yaliyofanyika jijini Mwanza.
Mhandisi Amboka amesema kwamba mpango kazi wa pamoja utaweza kufanikisha kutekeleza mpango huo ambao unaenda kumuongezea kipato cha ziada mwananchi wa kawaida na kumsaidia kuinuka kiuchumi.
“Kuna kazi za kwenda kufanya mtakaporudi kwenye maeneo yenu ya kazi na ili "mscore" vizuri lazima mkakae na wakufunzi wasaidizi na mtumie weledi wenu ili mfaulu utekelezaji wa mpango huu”.
Amesema kupitia CBRM serikali kupitia TARURA inatarajia kunusuru barabara nyingi hususan za vijijini ambazo zinawasaidia wananchi kufika mashambani msimu wa kilimo na pia kusafirisha mazao yao hata kama bado kuna mvua.
“Tanzania tuna mtandao mkubwa wa barabara, serikali inatafuta vyanzo mbalimbali vya kukwamua barabara zake na kuwafikia wananchi wake kwani barabara zinapoharibika wananchi hushindwa kupita na kupata huduma mbalimbali za kijamii”.
Hata hivyo, amesema mpango huo licha ya kuwaongezea kipato cha ziada mwananchi unaenda kuongeza umiliki wa miundombinu kwa wananchi ili kuondokana na dhana ya ulinzi wa miundombinu ni wa serikali bali wanaposhirikishwa katika matengenezo ya kawaida wataona barabara hizo ni mali yao na watazilinda na kuzitunza.
Awali akimkaribisha Kaimu Mtendaji Mkuu, Meneja wa Barabara TARURA, Mhandisi Oscar Mlekwa amewapongeza waratibu wa mpango huo kwa hatua kubwa waliofikia ambayo imeanza kuonesha mafanikio na kusema kuwa serikali inatupia macho kazi hizo ambazo zinajumuisha na kuwagusa wananchi na kuwainua kiuchumi.
Naye, Mratibu wa CBRM, Mhandisi Richard Missa amewaomba washiriki wa mafunzo hayo kutoa taarifa kwa makini na kwa wakati ili kuwezesha kufikia malengo ya mpango huo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Programu kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bw. Dampu Ndezako amesema mpango wa CBRM ni jitihada za serikali za kuondoa hali ya umaskini kwa wananchi wake wa chini kwa kutumia vikundi ambapo wananchi wanaenda kupata fursa ya kuzalisha kipato na kuweza kujitegemea.




Social Plugin