Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA YAHIMIZA VIJANA KUTUMIA FURSA ZA KIUCHUMI


Na Mwandishi Wetu-DODOMA

Wizara ya Viwanda na Biashara imewahimiza wananchi, hususan vijana na wajasiriamali, kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na taasisi zake ili kukuza biashara, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Wito huo umetolewa leo Juni 17, 2026 na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Saidi Msabimana, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Msabimana amesema wizara hiyo, ambayo ni miongoni mwa taasisi muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, imeshiriki maonesho hayo pamoja na taasisi nane zilizo chini yake kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi pamoja na kutoa elimu kuhusu biashara, viwanda na uwekezaji.

Amesema jukwaa hilo limetumika kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa kuwapa taarifa za huduma zinazotolewa na kuwaelekeza namna ya kutumia fursa zilizopo kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

“Tunatumia jukwaa hili kuwafikia wananchi moja kwa moja, kuwaeleza huduma tunazotoa na kuwahamasisha kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla,” amesema Msabimana.

Katika maonesho hayo, taasisi zilizo chini ya wizara hiyo zimeendelea kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za usajili wa biashara kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni Tanzania (BRELA), ambapo wananchi wamewezeshwa kupata huduma za usajili wa kampuni, majina ya biashara na alama za biashara kwa njia ya kidijitali.

Kwa upande wa Mamlaka ya Usajili wa Maghala Tanzania (ZAGARA), wananchi wanaomiliki au wanaotarajia kuendesha maghala wamepata elimu na huduma za usajili pamoja na leseni zinazotakiwa kisheria.

Aidha, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE ) kimetumia maonesho hayo kutoa taarifa za udahili na programu mbalimbali za masomo zinazolenga kuwaandaa vijana kuwa wataalamu na wajasiriamali wenye ushindani sokoni.

Vilevile, Wakala wa Vipimo umeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo katika biashara ili kulinda haki za walaji na kuimarisha uaminifu katika shughuli za kibiashara nchini.

Msabimana amesema kupitia maonesho hayo, zaidi ya wananchi 365 wamepata huduma za kuboresha mifumo ya biashara zao pamoja na taratibu za usajili wa lebo za bidhaa, hatua inayosaidia kuongeza ubora na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande mwingine, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), limeendelea kutoa taarifa kuhusu miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Liganga, Mchuchuma na Soda Ash, inayotarajiwa kuwa kichocheo cha mapinduzi ya viwanda, ajira na ukuaji wa uchumi.

Msabimana amewahimiza wananchi kutembelea mabanda ya wizara hiyo katika maonesho hayo ili kupata huduma, elimu na taarifa sahihi zitakazowawezesha kuboresha maisha yao na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi shindani wa Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com