Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mtaalamu wa kilimo na biashara ya kilimo kutoka Israel, Oran Reuveni, amesisitiza kuwa kilimo cha parachichi na embe nchini Tanzania kinahitaji kuendeshwa kwa usimamizi wa kisasa na wa kitaalamu ili kuongeza tija na ubora wa mazao.
Amesema hayo jijini Dodoma wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima, viongozi na wataalamu kuhusu usimamizi bora wa bustani za matunda kwa kutumia mbinu za kisasa.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na CultivAid yalifanyika katika shamba darasa la Kituo cha Ubunifu na Teknolojia ya Kilimo AITEC na yalilenga kuboresha ujuzi wa washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Washiriki wa mafunzo hayo walitoka mikoa 13 ya Tanzania, wakiwemo wataalamu kutoka TAHA, AMAGRO, NIRC na TARI.
Reuveni alieleza kuwa mafanikio ya bustani za matunda huanza kwa kuelewa uhusiano kati ya biolojia ya mti na mazingira yanayouzunguka, huku akisisitiza umuhimu wa kutambua vikwazo vya kimazingira vinavyoathiri uzalishaji.
Alitaja changamoto hizo kuwa ni upungufu wa maji, hali ya udongo, mabadiliko ya hali ya hewa, shinikizo la magonjwa na mapungufu ya miundombinu, akisema vinapaswa kushughulikiwa kwa mbinu za kitaalamu.
Pia alipendekeza suluhisho kama usimamizi wa taji la mti, mifumo bora ya umwagiliaji, matumizi ya matuta yaliyoinuliwa, uboreshaji wa udongo, uchaguzi sahihi wa miche na kinga dhidi ya upepo ili kuongeza uzalishaji.
Mtafiti kutoka TARI Makutupora, Felister Mpole, alisema eneo la Dodoma linafaa kwa kilimo cha matunda kama parachichi na embe kutokana na hali yake ya hewa, akihamasisha wakulima kuwekeza zaidi ili kuongeza kipato.
Naye mwakilishi wa TAHA, pamoja na mkulima kutoka AMAGRO, walieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia wakulima kuelewa soko linahitaji nini kabla ya kuzalisha, jambo litakalosaidia kuongeza ubora wa mazao na kukuza biashara ya matunda nchini.



Social Plugin