Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Kukamilika kwa mradi wa kimkakati wa Kituo cha Kubadilishia Njia za Usambazaji Umeme (Switching Station) na Transforma ya Kudhibiti Umeme katika eneo la Mbande, Wilaya ya Kongwa, kunatajwa kufungua ukurasa mpya wa uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa kati wa Tanzania.
Mradi huo uliotekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 10.5, unalenga kuongeza uhakika wa huduma ya umeme na kuweka mazingira bora kwa ukuaji wa shughuli za uzalishaji mali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo Juni 16, 2026, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema upatikanaji wa umeme wa uhakika ni nguzo muhimu ya maendeleo ya viwanda, biashara, kilimo cha kisasa na utoaji wa huduma za kijamii.
Amesema mradi huo utaimarisha usambazaji wa umeme katika Wilaya za Kongwa, Gairo, Chamwino na baadhi ya maeneo ya Mpwapwa, hatua itakayochochea uwekezaji na kuongeza tija katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya nishati ili kuhakikisha wananchi na wawekezaji wanapata huduma bora ya umeme inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye,” amesema Ndejembi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema mradi huo umeongeza uwezo wa mtandao wa umeme katika Mkoa wa Dodoma na maeneo ya jirani, huku ukiimarisha ubora wa huduma kwa watumiaji.
Kwa mujibu wa Twange, uwekezaji huo unatarajiwa kuvutia viwanda vipya, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na kuongeza fursa za ajira kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji na biashara.
Amesema ukuaji wa haraka wa Mkoa wa Dodoma kama Makao Makuu ya Nchi unahitaji miundombinu imara ya nishati, jambo linaloifanya TANESCO kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuongeza uwezo wa usambazaji wa umeme.
Mradi huo unatajwa kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi wa wananchi wa Kongwa na maeneo jirani, huku ukiweka msingi wa ukuaji wa sekta mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme wa uhakika.








Social Plugin