Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PAC YAIBANA TRA KUREKEBISHA MAPUNGUFU YA UKUSANYAJI KODI, YAAGIZA HATUA ZA HARAKA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuchukua hatua za haraka kurekebisha mapungufu yaliyoainishwa katika ukaguzi wa hesabu za taasisi hiyo, ikisisitiza kuwa ufanisi wa ukusanyaji wa kodi ni msingi muhimu wa kuimarisha mapato ya ndani na maendeleo ya taifa.

Maelekezo hayo yametolewa wakati wa kikao cha PAC kilichoongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Devotha Minja, kilichokutana na uongozi wa TRA kwa lengo la kupokea, kupitia na kuchambua taarifa ya hesabu za mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025, zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kamati hiyo imeitaka TRA kushughulikia kwa haraka dosari zote zilizobainishwa na CAG, hasa katika maeneo ya ukusanyaji wa kodi na usimamizi wa mapato ya serikali, ili kuhakikisha fedha zinazostahili kuingia hazipotei.

Aidha, PAC imeisisitiza TRA kuendelea kuimarisha mifumo yake ya usimamizi wa kodi kwa kuongeza ufanisi katika ukaguzi wa walipakodi, uhakiki wa taarifa pamoja na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa mapato ili kuongeza uwazi na tija katika ukusanyaji wa mapato ya umma.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema mamlaka hiyo imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na PAC na kwamba tayari imejipanga kuyatekeleza kwa wakati ili kuboresha utendaji wake.

Mwenda amesema TRA itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali kuhakikisha changamoto zilizobainishwa zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu na kuongeza ufanisi wa huduma kwa walipakodi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Uledi Mussa, amesema kikao hicho kimekuwa fursa muhimu ya kutathmini utendaji wa taasisi na kubaini maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu ili kuifanya TRA kuwa taasisi yenye ufanisi na inayoaminiwa zaidi na wananchi.

Amesema pamoja na kuimarisha mifumo ya ndani, TRA itaendelea kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari kama njia ya kuongeza mapato ya ndani na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Vilevile, ameiomba Kamati ya PAC kuendelea kuwa mshirika katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, akieleza kuwa ushiriki wa kila mdau ni nguzo muhimu katika kujenga uchumi imara na kuongeza uwezo wa serikali kugharamia huduma za kijamii na maendeleo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com