Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JAI YAWASILISHA CHANGAMOTO ZAKE KWA SPIKA WA BUNGE



Na mwandishi wetu,Dodoma

Jumuiya ya Akhlaaqul Islaam (JAI)imewasilisha rasmi kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu, ripoti inayoeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutafuta ufumbuzi na kuimarisha utendaji wake.

Akizungumza jana Jijini hapa Mratibu wa JAI Mkoa wa Dodoma, Ally Kanda, alisema viongozi wa jumuiya hiyo walipata fursa ya kutembelea Bunge kwa mwaliko wa Spika Zungu na kufanya mazungumzo yaliyolenga kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya taasisi hiyo.

Alisema katika ziara hiyo walikabidhi ripoti maalumu kwa Spika ikibainisha changamoto mbalimbali zinazokwamisha utekelezaji wa shughuli za JAI pamoja na mapendekezo ya namna ya kuzitatua.

"Kupitia mwaliko wa Mheshimiwa Spika, tulipata nafasi ya kutembelea Bunge na kukutana naye. Katika kikao hicho tulimkabidhi ripoti yetu inayoeleza changamoto zinazoikabili taasisi ya JAI na matarajio yetu katika kuzitatua," alisema Kanda.

Alifafanua kuwa ujumbe huo uliongozwa na Amir Mkuu wa JAI Taifa, Yahya Masau, ukiambatana na Naibu Amir, Sheikh Amani, Katibu wa JAI Taifa, Saad, pamoja na Mwanasheria wa jumuiya hiyo, Hassan Malanga.

Kanda alisema viongozi hao walieleza masuala mbalimbali yanayohitaji ushirikiano wa wadau na taasisi za Serikali ili kuimarisha huduma na shughuli zinazotekelezwa na JAI kwa manufaa ya jamii.

Aidha, alitoa shukrani kwa Spika wa Bunge kwa kuwapokea na kusikiliza maoni yao, huku akieleza matumaini kuwa mawasilisho yao yatapata ufumbuzi unaostahili.

"Tunamuomba Mwenyezi Mungu Allah (S.W.) ayapitishe yale yote tuliyoyawasilisha na kutusaidia kufanikisha malengo yetu kwa manufaa ya taasisi na jamii kwa ujumla," alisema Kanda.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com