Na mwandishi wetu,Dodoma
TANZANIA na Uturuki zimethibitisha upya dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya kilimo, sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Kilimo wa Tanzania wa mwaka 2050 na Ajenda ya 10/30, inayolenga kuifanya sekta hiyo kuwa yenye tija, ushindani wa kibiashara na kufikia ukuaji wa asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030.
Hayo yalibainishwa Juni 17, 2026 wakati wa majadiliano kati ya Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo na Balozi wa Jamhuri ya Uturuki nchini Tanzania, Bekir Gezer, yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Mazungumzo hayo yalibainisha maeneo muhimu ya ushirikiano, hususan katika miundombinu ya umwagiliaji, miradi ya matumizi ya mashine za kilimo, maghala ya kuhifadhia mazao baada ya kuvuna pamoja na msaada wa kiufundi katika kujenga uwezo.
Katika mazungumzo yao, Balozi Gezer alisifu diplomasia ya uchumi kati ya nchi hizo mbili, akibainisha kuongezeka kwa miradi ya Uturuki nchini Tanzania katika sekta za afya, elimu, uvuvi, nishati na biashara.
Pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kilimo katika kuboresha ustawi wa wakulima na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Ziara hii inaonesha dhamira ya Uturuki katika kufanikisha upya Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuimarisha ushirikiano wa kilimo. Ni vyema kutambua kuwa nchi zetu zilikuwa na MoU ya awali kuanzia mwaka 2009 hadi 2014, hivyo napongeza utayari wenu wa kuimarisha zaidi uhusiano wetu wa kiuchumi,” alisema Chongolo.
Viongozi hao wawili pia walijadili nafasi ya Shirika la Kimataifa la Ushirikiano na Maendeleo la Uturuki (TiKA), ambapo Balozi Gezer aliihamasisha Serikali ya Tanzania kutumia fursa za miradi ya TiKA kwa manufaa ya wakulima. Kwa upande wake, Waziri Chongolo alieleza fursa nyingine za uwekezaji ambazo nchi hizo zinaweza kushirikiana, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuhamasisha uongezaji thamani wa mazao, biashara ya kilimo na uchakataji wa mazao ya kilimo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu (Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula)Profesa Peter Msoffe, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao;Dk Yasinta Nzogela,
Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Usalama wa Chakula, Happy Pascal, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Kilimo; Tagie Daisy,
pamoja na wawakilishi kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Uturuki nchini Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Social Plugin