Na Wellu Mtaki, Dodoma

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia Kampuni Tanzu ya Ujuzi ya VETA, imefanikiwa kuzalisha bidhaa 825 ambazo tayari zimesambazwa katika taasisi mbalimbali za serikali pamoja na hoteli zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha matumizi ya ujuzi wa ufundi katika uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na thamani ya kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Meneja wa Kampuni Tanzu ya Ujuzi ya VETA, Mhandisi Marco Kapinga, amesema kampuni hiyo imeendelea kutumia maarifa na ujuzi unaopatikana kupitia mafunzo ya VETA kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya taasisi za umma, sekta binafsi na makundi tofauti ya jamii.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha namna mafunzo ya ufundi stadi yanavyoweza kuchangia moja kwa moja katika maendeleo ya uchumi wa nchi kupitia uzalishaji wa bidhaa na huduma zenye viwango vinavyokubalika sokoni.

“Lengo letu si tu kuzalisha bidhaa bora, bali pia kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa kisasa unaoweza kuwafanya washindane katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Tayari kuna fursa zinazojitokeza katika nchi mbalimbali ikiwemo Canada, ambazo zinahitaji wataalamu wenye stadi za ufundi,” amesema Mhandisi Kapinga.

Ameongeza kuwa kampuni hiyo imekuwa daraja muhimu la kuwawezesha wanafunzi na wahitimu wa VETA kupata uzoefu wa vitendo kupitia ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji, jambo linaloongeza uwezo wao wa kuajirika na kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao.

Kwa upande wake, Meneja wa Rasilimali Watu wa VETA, Eliaika Manyanga, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA, amesema bidhaa zinazooneshwa katika maonesho hayo zimetengenezwa na wanafunzi kwa kushirikiana na walimu wao kupitia mfumo wa mafunzo ya vitendo unaotolewa katika vyuo vya VETA nchini.

Amesema bidhaa hizo zinajumuisha vifaa mbalimbali vya matumizi ya nyumbani, ofisini na katika sekta nyingine za uzalishaji, ambavyo vinaonesha kiwango kikubwa cha ubunifu, umahiri na uwezo wa wanafunzi wa VETA katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi kupitia teknolojia na ujuzi wa ufundi.

“Bidhaa hizi ni ushahidi wa ubora wa mafunzo yanayotolewa na VETA. Wahitimu wetu wanapata ujuzi wa vitendo unaowawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokubalika sokoni na zinazoweza kushindana na bidhaa nyingine,” amesema Manyanga.

Aidha, ameeleza kuwa VETA inaendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu yanayolenga kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kuajirika katika sekta mbalimbali za uchumi. Amesisitiza kuwa taasisi hiyo inaendelea kuboresha mitaala na mazingira ya kujifunzia ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira linalobadilika kwa kasi.

Manyanga pia amebainisha kuwa udahili wa wanafunzi kwa muhula mpya utaanza mwezi Julai mwaka huu, huku akiwahimiza vijana kutumia fursa hiyo kujiunga na kozi mbalimbali za ufundi stadi zinazotolewa katika vyuo vya VETA vilivyopo nchini kote.

Sambamba na hilo, amefafanua kuwa usajili wa wanafunzi unafanyika kupitia mfumo maalumu wa kidijitali unaorahisisha waombaji kuwasilisha maombi yao na kupata nafasi katika kozi wanazozipendelea kwa haraka na kwa uwazi zaidi.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya huduma zinazotolewa na VETA, yenye lengo la kuongeza upatikanaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wengi zaidi na kuchangia juhudi za Serikali za kukuza ajira, ujuzi na maendeleo ya viwanda nchini.