Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya ya Uchaguzi, Bw. Ramadhan Kailima, amepongeza ufanisi na uwazi wa Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja unaosimamiwa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja, akieleza kuwa mfumo huo umechangia kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini.
Bw. Kailima alitoa pongezi hizo Juni 18, 2026 alipotembelea banda la PBPA katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kupata maelezo kuhusu utekelezaji wa mfumo huo, alisema kuwa umejengwa katika misingi ya uwazi na ushindani, jambo linalosaidia kupunguza gharama za uagizaji wa mafuta na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.
Akitoa ufafanuzi kwa mgeni huyo, Mkaguzi wa Mafuta wa PBPA, Bw. Issa Mwitazy, alisema kuwa katika mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja, ushindani hujikita katika gharama za usafirishaji wa mafuta (Premium).
Alieleza kuwa wazabuni hushindanishwa kwa kuwasilisha bei za usafirishaji wa bidhaa za petroli, dizeli na mafuta ya taa, ambapo mzabuni mwenye gharama nafuu zaidi hupatiwa zabuni husika.
“Utaratibu huu umetuwezesha kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha nchini wakati wote na wakati huohuo kuipa Serikali taarifa sahihi za kiasi cha mafuta na hivyo kuwezesha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na biashara ya mafuta,” alisema.
Aliongeza kuwa mikataba ya uagizaji wa mafuta husainiwa mapema kabla ya bidhaa kuwasili nchini, jambo linaloiwezesha Serikali kufanya makadirio sahihi ya mapato yatokanayo na sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Mwitazy, mafanikio ya mfumo huo yameifanya PBPA kuwa kitovu cha huduma za uagizaji mafuta kwa nchi kadhaa za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, zikiwemo Malawi, Rwanda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambazo huleta mahitaji yao kupitia mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja.
Ziara ya Bw. Kailima katika banda la PBPA ni sehemu ya shughuli za Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayolenga kuonesha mafanikio, huduma na ubunifu unaotekelezwa na taasisi za umma katika kuwahudumia wananchi na kuchangia maendeleo ya taifa.



Social Plugin