Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Ugunduzi wa mgodi mpya wa dhahabu katika Kata ya Dabalo, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, unatajwa kuwa fursa kubwa ya kiuchumi inayoweza kubadilisha maisha ya wananchi na kuongeza mapato ya Taifa, huku Serikali ikisisitiza uzingatiaji wa sheria za madini na tahadhari za kiusalama ili kuhakikisha rasilimali hiyo inanufaisha Watanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Dabalo katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi, akiwataka wachimbaji wadogo kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa na Serikali.
Senyamule amesema uwepo wa madini hayo ni neema kwa eneo hilo, lakini mafanikio yake yatategemea namna wachimbaji watakavyofuata sheria, kulipa kodi stahiki na kuchukua tahadhari dhidi ya watu wenye nia ovu wanaoweza kuhatarisha usalama wa mgodi na nchi kwa ujumla.
“Kunapokuwa na madini ya namna hii, tufuate taratibu za Serikali ili tuyatumie kwa tija, lakini tuwe na tahadhari nyingi za kiusalama. Tupokee wageni ambao wana tija na tusipokee wageni wenye hila kwa nchi yetu, huku tukizingatia pia huduma za afya kutokana na mikusanyiko inayoweza kujitokeza,” amesema Senyamule.
Ameongeza kuwa utii wa sheria za madini utasaidia kukuza uchumi wa wananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, huku ukiibua fursa mpya za maendeleo katika Kata ya Dabalo.
Mbali na masuala ya madini, Mkuu huyo wa Mkoa alikagua mradi wa maji uliotekelezwa na Shirika la World Vision Tanzania kwa gharama ya Shilingi 355,795,952.01 ambao umekamilika na kunufaisha wananchi wapatao 525 wa Kitongoji cha Muungano.
Pia ametembelea mradi wa umaliziaji wa maabara ya sayansi katika Shule ya Sekondari Dabalo uliogharimu Shilingi milioni 50 kutoka Serikali Kuu, ukiwa na lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia masomo ya sayansi pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaochagua mkondo huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja, amesema utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unaendelea vizuri, huku elimu kwa vitendo ikiendelea kutolewa kwa wakulima ili kuwahamasisha kupeleka zao la ufuta maghalani na kuuzwa kupitia mfumo rasmi unaowawezesha kupata bei yenye ushindani.
Amesema mwitikio wa wakulima umeendelea kuongezeka kutokana na uelewa wa faida za mfumo huo katika kuongeza kipato na kuimarisha tija kwenye sekta ya kilimo.





Social Plugin