Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ILO YATAKA HAKI ZA WAFANYAKAZI WAHAMAJI ZILINDWE


Na Mwandishi wetu, Mombasa

Shirika la Kimataifa la Kazi Duniani (ILO), limewataka Wanahabari wa Habari Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuandika habari zitakazolinda haki na heshima ya wahamaji wanaotoka nchi moja kutafuta kazi nchi nyingine.

Akifungua warsha ya kuwajengea uwezo viongozi  wa vyama vya wafanyakazi vya Wanahabari katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati Mshauri Mkuu wa kiufundi kutoka ILO, Aida Awel amesema bado kuna changamoto katika kuandika na kutangaza habari za wahamaji licha ya kuwa na mchango mkubwa wa kiuchumi.

"Wahamaji wamekuwa wakituma fedha kuchangia uchumi katika nchi zao na  wanazoishi lakini bado hawaandikwi vizuri," amesisitiza.

Warsha hiyo imeandaliwa na ILO kwa kushirikiana na Shirikisho la Wanahabari Afrika (FAJ), Shirikisho la Wanahabari Afrika Mashariki(FEAJ) na Chama cha Waandishi nchini Kenya (KUJ)  ambako kwa Tanzania imewakilishwa na viongozi wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA) akiwamo Mwenyekiti Taifa,Mussa Juma Siwayombe na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini Caren-Tausi Mbowe.

Akizungunzia idadi ya wahamiaji Awel amesema kwa sasa kuna zaidi ya wahamaji milioni 250 duniani ambapo Afrika pekee ina zaidi milioni 21 wakati Waafrika wanaoishi nje ya Afrika ni zaidi ya million 19.5.

"Afrika kwa mwaka inapokea zaidi ya Dola billion 100 karibu shilingi za Kitanzania trioni 262 kutoka kwa wahamaji jambo ambalo bado halitangazwi vizuri badala yake yanaandikwa  mapungufu zaidi."

"Sasa kuna Kombe la Dunia tunaona Waafrika wangapi wanachezea mataifa ya Ulaya na mabara mengine je,? Tunajua wanatuma nyumbani kiasi gani kila mwaka kutoka nchi moja hadi nyingine kutafuta kazi kwa kuzingatia sheria sio dhambi," ameongeza.

Naye rais wa Shirikisho la Wanahabari Afrika (FAJ), Omar Faruk Osman amewataka wanahabari kuacha upotoshwaji wanapoandika habari za uahamiaji 

Osman amesema uhamaji unasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana hivyo  jambo la muhimu ni kuwekewe mazingira mazuri ya kupata ajira .

"Serikali za Afrika zimekuwa zikitoa ahadi ya kupambana na changamoto ya ajira kwa Vijana lakini bado hazioni kujenga mazingira mazuri vijan kwenda nje ya nchi nyingine kufanya kazi halali ni fursa za kukabiliana na tatizo la ajira."

Awali rais wa Shirikisho la Wanahabari Ukanda wa Afrika Mashariki,(FEAJ), Eric Oduor amesema warsha hiyo itawawezesha viongozi wa wanahabari kurudi katika nchi zao kusaidia kuwajengea uwezo wanahabari kuhusiana na wahamaji.

Akizungumza katika Warsha hayo, Mwenyekiti WA JOWUTA,Mussa Juma ameshaur Serikali za Afrika kuwa na  sheria na sera rafiki ili kuwasaidia Vijana wakiwapo wanahabari kupata mikataba mizuri ya kazi katika nchi zao na nje ya nchi zao.

Warsha hii ya kikanda imehudhuriwa na viongozi wa vyama na mashirika ya wanahabari kutoka Comoro, Jibuti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com