Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAPIGA DEBE NA WAOKOTA MAKOPO DAR ES SALAAM, WAJITENGA NA MAANDAMANO YA 7/7



Vijana wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na waokota makopo, wapiga debe pamoja na wauzaji wa bidhaa baridi ikiwemo maji na soda katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam, wamekiri kushawishiwa mara kwa mara ili kushiriki katika maandamano yanayohamasishwa kufanyika Julai 07, 2026, wakiapa kutoshiriki tena katika maandamano yasiyokuwa rasmi kutokana na kile walichojifunza Oktoba 29, 2025.

Ripoti ya uchunguzi wa ghasia za Oktoba 29, iliyotolewa na Tume ya Rais iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande, pamoja na mambo mengine ilisema waandaaji wa ghasia za Oktoba 29, waliwashawishi vijana katika maeneo mbalimbali ikiwemo stendi za mabasi, kuweza kushiriki katika ghasia hizo na kutokana na ugumu wa maisha walipatiwa fedha kama kichocheo cha ushiriki.

Wakizungumza kwa sauti moja, vijana hao wamebainisha kuwa hawako tayari kutumika tena kama madaraja ya machafuko ambayo mwisho wa siku yanawaumiza wao wenyewe kiuchumi na kijamii, wakisisitiza kuwa utatuzi wa kero za wananchi unaofanywa na serikali katika ngazi mbalimbali ni jambo tosha kabisa na linalopaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania badala ya kuhamasisha matukio ya kuhatarisha amani ya Tanzania.

"Kila mtu anacho cha kujifunza Oktoba 29, kilichotokea kilimgusa kila mtu. Hatukuwahi na hatupaswi kuwa Nchi ya kufungiana ndani siku mbili au tatu. Naomba tutoe elimu pia kwa Vijana wengine, Oktoba 29 haikuwa siku ya kawaida na jambo lile halipaswi tena kujirudia." Amesema Bw. James Yuster, Mkurugenzi wa Taasisi binafsi ya James Foundation, yenye kusaidia watoto na Vijana wanaoishi katika mazingira magumu Nchini.

Wakati wa mazungumzo yao na Mwandishi wetu wa habari, Vijana hao akiwemo pia Bw. Julian Noah Kayuni, Mkazi wa Makongo juu,anayeuza maji na soda, wamewataka vijana wote nchini kukumbuka kwa umakini athari kubwa zilizotokea wakati wa machafuko ya Oktoba 29, 2025, wakitaka kumbukumbu hiyo chungu kuwa somo tosha kabla ya mtu yeyote kufanya maamuzi ya kukurupuka na kuingia barabarani bila kufikiria hatari ya mbele.

Msisitizo mkubwa umewekwa kwenye kulinda amani ya nchi ambayo ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, Vijana hao wakieleza kuwa bila amani hakuna yeyote anayeweza kufanya shughuli zake za kila siku, wakisema ni wajibu wa kila kijana kuwa mlinzi wa amani ya mwenzake ili kulinda mustakabali wa maisha yao na vizazi vijavyo, badala ya kuwa chanzo cha kubomoa nchi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com