Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NSSF YAFUNGUA MILANGO YA PENSHENI KWA MACHINGA NA BODABODA


Na Dotto Kwilasa, DODOMA

Habari njema kwa mamilioni ya Watanzania waliojiajiri. Kuanzia sasa, machinga, bodaboda, wakulima, mama lishe, wasusi na wavuvi wanaweza kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii NSSF na kupata pensheni, matibabu na mafao mengine.

Kauli hiyo imetolewa  Juni 15, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, wakati wa mafunzo maalumu kwa Waheshimiwa Wabunge.

Amesema Serikali imeanzisha *Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri* ili kuwajumuisha watu wa sekta isiyo rasmi ambao kwa muda mrefu wamechangia uchumi lakini hawakufikiwa na huduma za hifadhi ya jamii.

Nani anaweza kujiunga?

Bw. Mshomba amebainisha kuwa skimu hiyo inawalenga Watanzania wenye umri kati ya miaka 15 hadi 70, wanaoishi Tanzania Bara na kujishughulisha na shughuli za kujiajiri. Makundi yanayolengwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo, wafanyabiashara wa bodaboda, umachinga, mama lishe, wasusi na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Faida zipi?

Kwa kujiunga na skimu hiyo, mwanachama atapata kinga ya kiuchumi na kijamii ikiwemo mafao ya uzee, ulemavu, matibabu na msaada kwa familia iwapo mwanachama atakutwa na msiba.

Jinsi ya kujiunga:

Mkurugenzi huyo amesema mwananchi anayetaka kujiunga anatakiwa kutembelea ofisi yoyote ya NSSF au mawakala wake kote nchini kwa usajili. Wabunge wameombwa kutumia majukwaa yao kuhamasisha wananchi kuchangamkia fursa hii.

"Hii ni njia mojawapo ya Serikali kupunguza umaskini wa kipato, kuongeza tija na kujenga jamii yenye uhakika wa maisha bora ya baadaye," amesema Bw. Mshomba.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com