Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DODOMA YAPIGA HATUA KUELEKEA KIZAZI KISICHO NA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mkoa wa Dodoma umeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), ukiweka msingi imara wa kufikia azma ya kuwa na kizazi kisicho na maambukizi mapya (HIV Generation Zero).

Hatua hiyo imebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alipokutana na Rais na Mtendaji Mkuu wa Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF), Doris Macharia, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika sekta ya afya.

Katika mkutano huo, Mhe. Senyamule ameeleza kuwa Mkoa wa Dodoma una vituo vya afya 694 vinavyotoa huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za VVU na Kifua Kikuu. Alibainisha kuwa mafanikio yaliyopatikana ni makubwa na ya kutia moyo, yakionesha mwelekeo chanya katika kudhibiti maambukizi.

Amesema zaidi ya asilimia 102 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao za maambukizi huku asilimia 99.3 wako kwenye matibabu na asilimia 98 wamefanikiwa kufikia kiwango cha kudhibiti virusi mwilini.

Mafanikio haya yanaakisi juhudi za pamoja kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, hususan President's Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR) pamoja na EGPAF.

Kwa upande wake, Dkt. Macharia amesema EGPAF inaendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma za VVU na Kifua Kikuu katika vituo 153 kati ya 179 vinavyohudumiwa na shirika hilo mkoani hapa.

Ameeleza kuwa msaada huo unahusisha Mafunzo kwa wahudumu wa afya,Kuongeza muda wa utoaji huduma,Utoaji wa vifaa tiba na Kuimarisha rasilimali watu katika sekta ya afya.

Hatua hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma kwa wananchi.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa, Thomas Rutachuzibwa, amesema Mkoa utaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma za afya zinaimarishwa zaidi na hatimaye kutokomeza kabisa maambukizi mapya ya VVU.

Amesisitiza kuwa mafanikio yaliyopo yanapaswa kulindwa na kuendelezwa kwa kuongeza uwekezaji katika elimu ya afya, upimaji wa hiari pamoja na upatikanaji wa matibabu kwa wakati.

Kwa ujumla, hatua zinazochukuliwa na Mkoa wa Dodoma zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha sekta ya afya na kulinda ustawi wa wananchi. Ushirikiano thabiti kati ya Serikali na wadau wa maendeleo unaendelea kuwa chachu muhimu ya kufikia Tanzania isiyo na maambukizi mapya ya VVU.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com