Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinaunga mkono kikamilifu ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa matukio ya vurugu za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, na kiko tayari kushirikiana katika utekelezaji wa mapendekezo yote.
Akizungumza Dodoma Mei 4, 2026, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amesema tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kwa uhuru na weledi mkubwa, huku ripoti yake ikilenga kuimarisha umoja wa Taifa.
Amesema CCM inawashukuru Watanzania kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato huo na kusisitiza kuwa maridhiano ndiyo njia sahihi ya kuleta suluhu ya kudumu.
“Tutahamasisha wananchi kuunga mkono hatua hizi kwa ajili ya mshikamano wa kitaifa,” amesema Kihongosi.
Pia chama kimeunga mkono kuundwa kwa tume ya upelelezi kubaini chanzo cha vurugu na kuwawajibisha wahusika.
Kuhusu Katiba Mpya, amesema ni ajenda muhimu ya Chama hicho iliyo kwenye ilani ya 2025/2030 na mchakato wake unatarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2030.
Ametumia nafasi hiyo kuwa taka Vijana kuepuka vurugu na kuwa walinzi wa amani ya nchi.
Kwa upande mwingine, Kihongosi amemjibu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, John Heche, akisema UVCCM imeendelea kuzalisha viongozi wengi wa kitaifa.
Aidha, akizungumzia suala la Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, aliwataka Chadema kujitathmini kuhusu uanachama wake wa awali na si kukurupuka.

Social Plugin