Na Dotto Kwilasa
Naongea na mabinti wanaoumizwa kimya kimya na wanaume wenye ndoa wanaojua kutumia maneno matamu kuwafanya wajisikie wanapendwa kumbe wanatumiwa tu kupitisha muda na kutimiza matamanio yao.
Unakuta mwanaume ana mke wake, ana familia yake, lakini kwako anakuja na ahadi tamu, anakupangia maisha na kukufanya uamini wewe ndiye mwanamke wa ndoto zake.
Cha kusikitisha zaidi, anataka umuweke yeye kama “mume wa maisha” wakati yeye mwenyewe hawezi hata kukupa nafasi sawa na anayompa mke wake.
Mwisho wa siku mabinti wengi wanapoteza muda wao, wanaharibu future zao na kujikuta wamewekeza hisia zao kwa mwanaume ambaye hana mpango wa kuwapa maisha wanayostahili.
Kuna wanaume wana kipaji kikubwa cha kuigiza mapenzi. Anakutafuta kila siku, anakupigia simu usiku kucha, anakwambia wewe ndiye mwanamke anayempa furaha, lakini ukweli ni kwamba bado anaishi maisha yake ya kawaida na mke wake huku wewe ukipewa mabaki ya muda, mabaki ya hisia na wakati mwingine mabaki ya vitu.
Cha kushangaza zaidi, mwanaume huyo huyo anaweza kukuzuia usiwe na future na mwanaume mwingine.
Hataki uolewe, hataki uongee na wengine, hataki hata upost picha inayoweza kuwavutia wanaume wengine. Anakufanya ujisikie kama tayari wewe ni “mke wake”, wakati kiuhalisia wewe ni sehemu ya siri katika maisha yake.
Wasichana wengi wanaingia kwenye mtego huu kwa sababu ya maneno matamu na attention ya muda. Wanaacha malengo yao, wanaharibu future zao na kujikuta wanamjenga mwanaume ambaye hata hajawahi kuwaza kuwapa nafasi halisi maishani.
Ukweli mchungu ni huu… mwanaume anayokupenda kwa dhati hawezi kukuweka kwenye kivuli.
Kuna wengine wanafikia hatua ya kujifanya wanajali sana. Labda simu yako imeharibika au huna kabisa, lakini badala ya kukununulia mpya, anaenda kumnunulia mke wake simu mpya kisha anakuletea wewe ile ya zamani. Halafu bado anataka uchukulie hilo kama “upendo mkubwa”.
Jiulize… kama kweli wewe ndiye muhimu kwake, kwanini kila kitu kizuri kinaanzia kwa mke wake halafu wewe unapewa kilichobaki?
Mapenzi ya kweli hayatoi mabaki. Hayakufanyi ujifiche. Hayakufanyi usiwe na future yako mwenyewe.
Binti, jifunze kumuweka mwanaume kwenye nafasi yake. Sio kila anayesema “nakupenda” anastahili moyo wako. Wengine wanataka tu kukutumia kujaza upweke wao huku wakilinda familia zao kwa nguvu zote.
Usikubali kuwa sehemu ya maisha ya mwanaume ambaye hawezi kukupa nafasi ya kwanza mbele ya dunia. Kama anakufanya uwe siri, ujue tayari kuna anayeheshimiwa kuliko wewe kwenye maisha yake.
Mwanaume anayekupenda kweli atakujenga, atakulinda na atakupa heshima yako sio kukuweka waiting list ya mapenzi yasiyo na mwisho.

Social Plugin