Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAHARAKATI WAASWA KUUNGA MKONO RIPOTI YA MATUKIO YA OKTOBA 29, WAHIMIZWA KUJENGA TAIFA KWA HOJA ZA KITAALAMU



Na mwandishi Maalum, Dar

Mwanachama wa CHADEMA Odero Charles amewaasa Wanaharakati nchini kutumia kalamu zao na majukwaa ya mitandao ya kijamii kwa weledi na uzalendo katika kuielezea ripoti ya matukio ya Oktoba 29, 2025 iliyosomwa na kuwasilishwa rasmi leo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza kufuatia uwasilishaji wa ripoti hiyo,Odero amesisitiza kuwa nyaraka hiyo ni hatua muhimu katika kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, akiwataka wadau mbalimbali hasa wanaharakati na watumiaji wa mitandao kuitumia fursa hiyo kuhabarisha umma kwa usahihi na kwa kuzingatia taaluma badala ya kukisia au kupotosha ukweli.

Ameeleza kuwa kama kuna maeneo yenye mapungufu, basi yapingwe kwa hoja zenye vigezo na ushahidi wa kitaalamu, jambo litakalosaidia kuboresha mifumo ya utawala na haki badala ya kuchochea taharuki au migawanyiko isiyo na tija kwa taifa.

Aidha, amesisitiza kuwa huu si wakati wa kubaguana, kulaumiana au kuitana majina yasiyofaa, bali ni muda wa Watanzania kuunganisha nguvu na kusonga mbele kwa pamoja katika kujenga taifa imara lenye mshikamano.

Amesema hakuna taifa lingine litakalokuja kujenga Tanzania zaidi ya Watanzania wenyewe, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu katika kulinda amani na umoja wa nchi.

Katika muktadha huo, amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kuongoza kwa hekima na ustahimilivu kupitia falsafa yake ya 4R ambayo ni Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga Upya Taifa (Rebuilding), akisisitiza kuwa misingi hiyo imekuwa nguzo muhimu katika kuleta utulivu na mwelekeo chanya wa maendeleo nchini.

Vilevile, ametumia nafasi hiyo kumsihi Rais Samia kuendelea kudumisha moyo huo wa 4R kwa kufungua zaidi milango ya majadiliano ikiwemo kuangalia uwezekano wa kutoa msamaha kwa baadhi ya vijana waliokutwa na hatia kufuatia matukio ya Oktoba 29, ili kuimarisha maridhiano na kulirejesha taifa katika umoja wake.

Amesisitiza kuwa kwa sasa taifa linahitaji mjadala wa hoja, si mivutano ya hisia ikiwa ni pamoja na umoja bila migawanyiko ikiwa ni sehemu ya safari ya pamoja ya kuijenga Tanzania yenye amani, haki na maendeleo endelevu.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com