Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC KISHAPU AKAGUA MIRADI YA MAJI,AFYA,ELIMU NA UPANDAJI MITI, ASISITIZA UWAJIBIKAJI

Na Sumai Salum-Kishapu


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amepongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta za afya, elimu na maji.


Mhe. Masindi ametoa pongezi hizo kufuatia ziara yake ya kikazi iliyofanyika Aprili 23, 2026 katika Kata ya Kishapu na Mwataga ambapo ametembelea miradi mbalimbali ikiwemo Shule ya Msingi na Sekondari Isoso,Mradi wa maji ya Ziwa Ziwa Victoria kutoka Mhunze–Mwataga ulioko Shule ya Sekondari Mwataga, pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Dkt. Jakaya Kikwete.


Katika ziara hiyo, miradi iliyotembelewa ni pamoja na:

   1: Ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa ya awali na matundu 6 ya vyoo katika Shule ya Msingi Isoso, wenye thamani ya shilingi 71,800,000/=.

   2: Ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa ya elimu ya msingi, jengo la utawala, matundu 12 ya vyoo, pamoja na vyumba 2 vya madarasa ya awali na matundu 6 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Isoso, wenye thamani ya shilingi 342,900,000/=.

    3: Ununuzi wa dawa na vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wenye thamani ya shilingi 100,000,000/=.

    4: Utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria (Kishapu–Mwataga) wenye thamani ya shilingi 250,951,240/=.

    5: Mradi wa upandaji miti katika Shule ya Sekondari Isoso.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi,akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua miradi mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, Maji na upandaji miti Kata ya Kishapu na Mwataga wilayani humo Aprili 23, 2026


                              ELIMU

Mkuu huyo wa Wilaya amemtaka mhandisi wa Halmashauri na wasimamizi wote wa mradi wa vyumba viwili vya madarasa ya awali Shule ya msingi Isoso  wahakikishe yanakamilika siku 7 kuanzia leo ili wanafunzi hao waanze kuyatumia, huku akihimiza uanzishwaji wa ujenzi wa uzio katika shule hizo uwekwe kwenye mpango.


"Serikali yetu imedhamilia kuondoa adha kwa wanafunzi ndio maana inaleta fedha nyingi kuboresha miundombinu hivyo tuhakikishe tunasimamia miradi yote ya elimu kwenye Wilaya yetu na ikamilike kwa ubora na kwa muda uliopangwa hatutaki kusikia mkandarasi anamiradi mingi hivyo anashindwa kukamilisha kwa wakati uliopangwa" amesisitiza Masindi

                             MRADI WA AFYA 

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Mohamed Mkumbwa, amesema kuwa maboresho ya miundombinu ya afya yaliyofanywa na serikali yamechangia kupunguza rufaa na kuwezesha hospitali kutoa huduma mbalimbali, kufanya upasuaji mkubwa ikiwa ni pamoja na upasuaji wa utumbo kujikunja na tezi dume, pamoja na kuanzisha vitengo vipya vya huduma.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Masindi amewapongeza wasimamizi wa miradi kwa kazi nzuri wanayoifanya. Aidha, amepongeza Hospitali ya Dkt. Jakaya kwa kupunguza vifo vya watoto kutoka 17 hadi 5 katika robo iliyopita, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na kuboreshwa kwa vifaa tiba pamoja na ongezeko la wataalamu.


Masindi amewataka watumishi kusimamia kwa nidhamu matumizi ya vifaa tiba ili viwanufaishe walengwa waliokusudiwa. Alisisitiza kuepuka wizi wa dawa, kutobambikiza bili kwa wateja wa bima, pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa dawa ili kuondoa zilizoharibika. Pia alihimiza utoaji wa huduma kwa lugha nzuri na yenye staha kwa wateja.

                              MAJI

Katika sekta ya maji, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwataga, Grace Dionis na Belshazzar Jeremia, wameishukuru serikali kwa utekelezaji wa mradi wa maji katika kijiji chao, wakieleza kuwa umekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla. Wamesema mradi huo umesaidia kuondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali ambayo ilikuwa ikiathiri usalama wao pamoja na kupunguza muda wa kuhudhuria masomo kwa wakati.


Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Mwataga, Fikina Mathias, amesema upatikanaji wa maji pamoja na huduma ya chakula shuleni umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza utoro miongoni mwa wanafunzi na kuongeza kiwango cha ufaulu darasani licha ya kuwa bado baadhi ya wanafunzi wanakabiliwa na kutoka umbali mrefu Vijiji vya Migunga, Mwamagembe na Mwanulu.

         MRADI WA UPANDAJI MITI


Wilaya ya Kishapu kwa Msimu wa mwaka 2025/2026  jumla ya miche ya miti 1, 068,325 imepandwa ikihusisha miti ya mbao,matunda na  kivuli kwenye maeneo ya watu binafsi,taasisi za umma shule na maeneo ya watu binafsi huku TFS ikitoa miche (155,000), Halmashauri (90,000),TCRS (23,325), WDL(500,000), Kikundi cha kuhifadhi mazingira Maganzo(100,000) na watu binafsi (200,000).


Katika hatua nyingine, Mkuu huyo amewapongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani humo pamoja na Idara ya Misitu ya Halmashauri ya Kishapu  kwa juhudi zao za kugawa miche ya miti. Akisisitiza umuhimu wa kuendelea kupanda miti kwa wingi ili kurejesha uoto wa asili na kukabiliana na ukame unaoikabili Wilaya hiyo.


Mhifadhi Misitu kutoka wakala wa huduma za misitu TFS wilayani Kishapu Tumaini Masatu, ameeleza kuwa miti ina mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira, kuzuia mmomonyoko wa udongo na ukame,kuongeza uoto wa asili na hifadhi za misitu, kulinda vyanzo vya maji na kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amehimiza jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.


Aidha, Halmashauri ya Wilaya imepokea kiasi cha shilingi milioni 36 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upandaji miti katika shule za msingi, sekondari, taasisi za dini na za serikali, ikiwa ni sehemu ya mradi wa miaka miwili wa kuhifadhi mazingira.


Ziara hiyo imeacha alama ya ufuatiliaji fedha za serikali namna zinavyotumika kutekeleza miradi elekezi, ukamilishaji wa miradi kwa wakati na uwajibikaji wa watumishi waliobeba dhamana ya kusimamia mipango ya serikali.

Diwani wa Kata ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Joel NdettosonDiwani wa Kata ya Mwataga wilayani  Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.  Ponsian MatungwaMhifadhi misitu kutoka wakala wa huduma za misitu TFS wilayani Kishapu Tumaini MasatuMwalimu Mkuu Shule ya Msingi Isoso Gilbert MtungujaMkuu wa Shule ya Sekondari Isoso Annunsiatha Audax.     Meneja wa RUWASA wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Mhandisi Dickson KamazimaMfamasia Hospitali ya Dkt. Jakaya Kikwete wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Aurelia KadindeMganga Mfawidhi Hoapitali ya Dkt. Jakaya Kikwete wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Dkt. Mohamed MkumbwaMwanafunzi wa shule ya sekondari Mwataga Kata ya Mwataga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Belshazzar JeremiaMkuu msaidizi shule ya Sekondari Mwataga Fikina MathiasMwanafunzi wa shule ya sekondari Mwataga Kata ya Mwataga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Grace Dionis 





















































































































































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com