Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SATCO : SAFARI INAYOANZA NA UTU, SIO PESA TU



Na Dotto Kwilasa - Malunde 1 blog, Dodoma

Safari ya usiku ya tarehe 15 Machi 2026 kutoka Geita (Kalangalala) kwenda Dodoma  kupitia basi la SATCO EXPRESS, namba T 301 EHZ, imenipa funzo muhimu kuhusu maana halisi ya huduma bora kwa abiria katika usafiri wa mabasi ya masafa marefu.

Kwa tiketi yenye jina la Dotto Kwilasa, siti D1, nauli ikiwa shilingi 55,000, safari hii haikuwa tu ya kufika kutoka sehemu moja kwenda nyingine, bali ilikuwa uzoefu ulionionesha tofauti kati ya usafiri wa kawaida na huduma inayoweka utu wa abiria mbele.

Kuanzia kwa kondakta hadi dereva wa basi hilo, wahudumu wote walionyesha nidhamu, heshima na ukarimu wa hali ya juu kwa abiria.

 Ni wazi kwamba tabia ya wahudumu mara nyingi huamua hata namna abiria wanavyojihisi na kuendesha safari yao.Hii ina maana Wahudumu wanapokuwa na roho ya huduma na uvumilivu, hata abiria hujenga mazingira ya utulivu na heshima ndani ya basi.

Kilichonigusa zaidi katika safari hiyo ni namna walivyokuwa wakizingatia usalama wa abiria, hasa kwa wale waliokuwa wanashuka njiani wakati wa usiku. Badala ya kusimamisha basi na kuondoka mara moja, dereva alikuwa anahakikisha kwanza abiria anayeshuka anakuwa katika mazingira salama.

Katika baadhi ya maeneo ambayo ni vijiji vya giza au sehemu za porini, dereva na kondakta walikuwa wakimwambia abiria kwa uwazi: “Piga simu kwanza aje mtu wa kukuchukua, hatuwezi kukuacha hapa hivi hivi.”

Kitendo hicho kilionesha kiwango kikubwa cha uwajibikaji na kujali maisha ya abiria, jambo ambalo si rahisi kulikuta katika baadhi ya mabasi mengi ya safari ndefu.

Uzoefu huu ulinikumbusha tukio la miezi miwili iliyopita niliposafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa basi lingine maarufu. Nilipofika eneo la Mtumba – Mji wa Serikali, nilihitaji kushuka ili niweze kujiandaa kuwahi kazini asubuhi iliyofuata. 

Hata hivyo, niliwekewa ugumu kushuka kwa madai kwamba sehemu ile si kituo cha basi na hatimaye nikapitilizwa hadi Nane Nane Stand kwa lazima.

Hali hiyo ilinilazimu kuanza tena kutafuta usafiri wa kurudi nyuma , jambo lililonisababishia usumbufu mkubwa na kunifanya nishindwe hata kufika nyumbani kujiandaa vizuri kuwahi kazini.Malengo yangu ya kusafiri usiku yakawa hayana maana tena. 

Ndiyo maana safari ya jana imenionyesha tofauti kubwa. Kwa SATCO, inaonekana wazi kuwa usafiri si suala la biashara pekee, bali ni huduma inayohusisha utu na heshima kwa abiria.

Mbali na hilo, jambo lingine lililovutia ni utaratibu wa kutoa elimu kwa abiria kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira, pamoja na kuanza safari kwa sala. 

Hii inaonyesha kuwa safari haijengwi tu kwa uendeshaji wa gari, bali pia kwa maadili na utamaduni wa kuwajali watu.

Cha kushangaza zaidi, hata pale basi liliposimama kwa ajili ya kumshusha abiria, hakukuwa na malalamiko kutoka kwa abiria wengine. Hakusikika lugha za kukereka au kauli za kukimbizana kama zinavyotokea katika safari nyingine.

Badala yake, kulikuwa na utulivu na heshima miongoni mwa abiria wote. Ni kana kwamba ule ukarimu wa wahudumu uliambukiza hata abiria wenyewe.

Cha kuvutia zaidi ni kwamba pamoja na kusimama kwa tahadhari na kuzingatia usalama wa abiria, bado tulifika Dodoma kwa wakati na sawa kabisa na mabasi mengine yanayodhaniwa kuwa na kasi zaidi.

Huu ndio mfano halisi wa huduma ya kitaalamu yenye ubinadamu.

Ujumbe wa simulizi hii si kusifia , bali kukumbusha umuhimu wa kuheshimu na kuwajali abiria katika sekta ya usafiri. Kwa bahati mbaya, bado kuna baadhi ya makonda au wahudumu wa mabasi ambao hutumia lugha zisizofaa au kuwa na tabia za kunyanyasa abiria.

Lakini katika safari hii, SATCO imeonyesha kuwa inawezekana kutoa huduma bora, yenye heshima na utu bila kupoteza ufanisi wa safari.

Kwa hakika, mmiliki wa mabasi ya SATCO ana sababu ya kujivunia wafanyakazi wake. Nidhamu yao, utu wao na namna wanavyowajali abiria inaonyesha wazi kuwa wamejengewa misingi imara ya huduma kwa wateja.

SATCO imeonyesha kuwa usafiri bora haupimwi kwa kasi ya gari pekee, bali kwa namna unavyowathamini na kuwalinda watu wanaotumia huduma hiyo.

Hongereni SATCO kwa kuendelea kuonyesha mfano wa usafiri salama na wenye utu kwa abiria.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com