Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Seleman Msumi, amesema kuwa malezi bora kwa watoto ni nguzo muhimu katika kuhakikisha jamii inapata maendeleo endelevu na yenye ustawi.
Amesema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali ili kuhakikisha mwongozo wa malezi bora unatekelezwa kwa ufanisi katika jamii.
Aidha, amesema ushirikiano huo utasaidia kupunguza vitendo vya ukatili vinavyotokea katika jamii, hasa kwa watoto, kwa kuwa jamii itakuwa na uelewa mpana kuhusu wajibu wa malezi na ulinzi wa mtoto.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Victor Rugarabamu, amelipongeza shirika la SOS Children’s Village kwa juhudi zake za kuanzisha vikundi vya malezi katika mkoa wa Arusha.
Pia Rugarabamu amesema vikundi hivyo vina mchango mkubwa katika kuhamasisha na kuimarisha malezi bora, pamoja na kuongeza uelewa kwa jamii juu ya haki na ustawi wa mtoto.
Pia katika kongamano hilo, Meneja wa SOS Children’s Village mkoa wa Arusha, Mpeli Kalonge, amesema kuwa lengo la shirika hilo ni kutoa malezi mbadala kwa watoto wanaohitaji msaada, pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto na kupinga vitendo vya ukatili katika jamii.
Naye Veronika Kidemi, ambaye ni mmoja wa waathirika wa vitendo vya ukatili, ameitaka jamii kupaza sauti na kushirikiana kwa pamoja kupambana na matukio ya ukatili yanayotokea katika jamii ili kulinda haki na usalama wa watoto na makundi mengine yaliyo hatarini.




Social Plugin