
Na Simeo Makoba _ Shinyanga
Askofu mteule wa jimbo jipya Katoliki la Bariadi, Mhashamu Prosper Baltazar Lyimo, kesho Jumanne tarehe 17, Machi, 2026, atapokelewa katika Jimbo la Shinyanga akitokea jimboni Arusha.
Askofu Lyimo atapokelewa majira ya mchana katika kijiji cha Welezo kilichopo eneo la Mto Manonga mpakani mwa Jimbo kuu la Tabora na Jimbo la Shinyanga.
Akiwa katika eneo hilo, Askofu Lyimo atabusu ardhi ikiwa ni ishara ya upendo wake kwa Jimbo la Shinyanga ambalo ndilo Jimbo Mama wa Jimbo teule la Bariadi, na baadaye msafara wake utaelekea moja kwa moja katika makazi ya Askofu wa Jimbo la Shinyanga kwa mapumziko.
Asubuhi siku ya Jumatano tarehe 18, Machi, 2026, msafara wa Askofu Lyimo utaondoka kuelekea katika Jimbo teule la Bariadi, ambapo atapokelewa katika kijiji cha Zanzui kilichopo Kilometa chache kabla ya kufika kwenye eneo la mto Simiyu, mpakani mwa Jimbo la Shinyanga na Jimbo teule la Bariadi.
Askofu Lyimo atakwenda moja kwa moja mjini Bariadi katika Kanisa kuu la muda la Mtakatifu John na kutoa heshima kwa Sakramenti ya Ekaristi takatifu na baadaye saa 11:00 jioni atashiriki Ibada ya masifu ya jioni , ambayo ni sehemu ya uanzishwaji wa Jimbo jipya la Bariadi.
Askofu Lyimo atasimikwa rasmi kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo jipya la Bariadi Alhamisi tarehe 19, Machi, 2026, kupitia adhimisho la Misa takatifu ambayo itafanyika kwenye uwanja wa Halmashauri mjini Bariadi.
Askofu Lyimo ambaye alikuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Arusha, aliteuliwa na Baba Mtakatifu Leo XIV, kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Jipya la Bariadi mnamo tarehe 08, Januari, 2026.
Jimbo jipya la Bariadi limeanzishwa baada ya kugawanywa kwa jimbo la Shinyanga, ambalo hapo awali lilikuwa linachukua eneo lote la mkoa wa Simiyu na wilaya zote za mkoa wa Shinyanga isipokuwa tu Wilaya ya Kahama ambayo inaunda jimbo linalojitegemea (Jimbo Katoliki la Kahama) ambalo liko chini ya Metropolitani ya Tabora.
Social Plugin