Na Sumai Salum – Kishapu
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kulirejesha zao la pamba katika hadhi yake ya kihistoria na kiuchumi, huku mkulima akiwekwa mbele katika mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji wenye tija na kuinua maisha ya wakulima.
Hatua hiyo imebainishwa Februari 4, 2026 wakati wa kikao maalum cha Kamati ya Mazao Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kilichofanyika katika Ukumbi wa SHIRECU, kikilenga kusikiliza changamoto zinazokabili zao la pamba na kuweka mikakati sahihi na ya pamoja katika uboreshaji wa uzalishaji, masoko na manufaa ya moja kwa moja kwa mkulima.
Kikao hicho ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kulifanya zao la pamba kuwa zao la kimkakati linalochangia kikamilifu uchumi wa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Kamati hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, huku kikao hicho kikiendeshwa na mwakilishi wake, Afisa Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Fadhili Joseph Mvanga.
Akizungumza katika kikao hicho, Mvanga amesisitiza kuwa Serikali inalenga kuimarisha mifumo ya uzalishaji, pembejeo, usimamizi na masoko ili mkulima apate faida halisi, sambamba na kurejesha imani ya wakulima katika zao la pamba.
"Ili tufikie dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Samia Suluhu katika kuimarisha maisha ya mkulima kupitia mazao ya kimkakati ikiwemo pamba, nihimize kuwepo ufuatiliaji wa karibu, mawasiliano ya mara kwa mara kati ya maafisa ugani na wakulima, pamoja na utoaji wa elimu kwa wakati ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo" ameongeza Mvanga.
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kishapu, Shija Malisha Ntelezu na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Josephat Limbe, wameiomba Bodi ya Pamba Tanzania kuzingatia ombi la Wilaya la kuruhusu uwepo wa wanunuzi zaidi ya mmoja wa zao la pamba, hatua itakayoongeza ushindani wa masoko, kuimarisha bei na kumpa mkulima uhakika wa faida kuelekea msimu wa uzalishaji wa 2026/2027.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Marco Mtunga, ameihakikishia Wilaya ya Kishapu kuwa Serikali inaendelea kuboresha sera, usimamizi na ushirikiano na wadau ili kuimarisha soko la pamba na kuhakikisha mkulima analindwa dhidi ya changamoto za bei na masoko.
Balozi wa zao la pamba, Aggrey Mwanri, akizungumza katika kikao hicho ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha elimu, teknolojia na ubunifu vinatumika ipasavyo ili kulifanya zao la pamba kuwa la kisasa, lenye tija na linalomlipa mkulima stahiki yake.
Hata hivyo Wilaya ya Kishapu imebainisha mafanikio makubwa yaliyofikiwa mpaka sasa katika maandalizi ya msimu wa pamba, ikiwemo upatikanaji wa tani 2,555 za mbegu za pamba, viuatilifu 264,232 kati ya 840,000 vinavyotarajiwa, pamoja na mbolea hai lita 20,200 sawa na asilimia 80 ya mapipa na matenki yaliyonunuliwa na makampuni husika.
Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya uzalishaji kwa kuwezesha trekta 19, maafisa wa mpango wa BBT 78 wakiwa na pikipiki 74, pamoja na vifaa vya kisasa vya kunyunyizia viuatilifu ikiwemo Boom Sprayers 3 na Drones 9, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza gharama kwa mkulima.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wadau mbalimbali wa zao la pamba wakiwemo maafisa wa BBT, wanunuzi wa pamba, viongozi wa AMCOS, maafisa ugani na madiwani, hatua inayodhihirisha mshikamano wa pamoja katika kulijenga na kulirejesha zao la pamba kama nguzo muhimu ya uchumi wa Wilaya ya Kishapu.
Social Plugin