
Mbunge Mteule wa Jimbo Jipya la Itwangi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Azza Hillal Hamad, amepongeza shule tatu za msingi zilizopo jimboni humo kwa kufanya vizuri katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2025, akisema matokeo hayo ni kielelezo cha juhudi, nidhamu na ushirikiano mzuri kati ya walimu, wazazi na wanafunzi.
Shule zilizong’ara ni Shule ya Msingi Masunula ya Kata ya Usule, Shule ya Awali na Msingi OLA ya Didia, na Shule ya Msingi Sumbigu ya Kata ya Bukene ambazo zote zimeonyesha kiwango cha juu cha ufaulu na kuibua matumaini mapya kwa maendeleo ya elimu katika Jimbo la Itwangi.
Katika matokeo hayo, Shule ya Msingi Masunula imeweka historia kwa wanafunzi wake wote kupata daraja “A”, ikijipatia sifa kama miongoni mwa shule bora kitaifa.
Vilevile, Shule ya Awali na Msingi OLA imefanikiwa kwa wanafunzi wake wote kupata ufaulu wa juu, huku Shule ya Msingi Sumbigu ikionesha matokeo mazuri kwa wanafunzi wake kupata madaraja “A” na “B”.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Mhe. Azza Hillal Hamad amewapongeza walimu na viongozi wa shule hizo kwa kujituma, akiwataka kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata elimu bora yenye matokeo chanya.
Ameongeza kuwa matokeo haya yanadhihirisha kwamba Jimbo la Itwangi lina uwezo mkubwa wa kuongoza kitaifa katika elimu, endapo kila upande utaendelea kujituma na kushikamana katika kutimiza malengo ya maendeleo ya sekta hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), shule hizo zimekuwa miongoni mwa zinazofanya vizuri zaidi katika Wilaya ya Shinyanga, jambo linaloipa heshima kubwa elimu ya jimbo hilo jipya.
🔗 Fungua Link kuona matokeo ya shule hizi:
Matokeo ya Shule ya Msingi Masunula
Matokeo ya Shule ya Awali na Msingi OLA
Matokeo ya Shule ya Msingi Sumbigu



Social Plugin