MKURUGENZI WA BODI YA KOROSHO ATUMBULIWA


Waziri wa wizara ya kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Dodoma, Jumamosi 21 Aprili 2018. 
****
Waziri wa wizara ya kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe kusitisha mkataba wa kazi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania Ndg Hassan Jarufo.

Waziri Tizeba ametoa agizo hilo kwa katibu mkuu wa wizara hiyo leo Jumamosi 21 Aprili 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Dodoma ikiwa ni muda mchache mara baada ya kumalizika kwa dhifa ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa.

Akielezea sababu za kuagiza kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi huyo, Mhe. Dkt Tizeba alisema kuwa hayo yamejili baada ya kuangalia mwenendo wa Ndg Jarufo na kutafakari jinsi zao la korosho linavyoendeshwa, ikiwa ni pamoja na kutoridhishwa na upatikanaji wa viuwatilifu kwa wakati.

Aidha, Mkataba huo umesitishwa kuanzia leo tarehe 21 Aprili 2018 hivyo Katibu Mkuu wa wizara hiyo atapaswa kufanya taratibu zote za kiutumishi ikiwa ni pamoja na kumpatia taarifa haraka muhusika na utekelezaji wake kuanza haraka.

Alisema ndani ya muda mfupi Wizara ya kilimo itamtangaza Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo ili kuchukua nafasi hiyo kuendeleza kusimamia sekta hiyo.

“Hizi hatua tunazochukua ni kuhakikisha kuwa wadau wakubwa wa korosho ambao ni wakulima wanaendelea kunufaika na zao lao, hivyo wakulima wasiwe na wasiwasi kwani pamoja na kuondolewa Mkurugenzi huyo lakini shughuli za serikali zitaendelea kama kawaida na maslahi yao yatasimamiwa ipasavyo” Alikaririwa Mhe. Dkt Tizeba.



Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527