VIONGOZI WA KIJIJI MBARONI KWA KUKODISHA MASHAMBA KWA RAIA WA BURUNDI KIGOMA

Kamati ya ulinzi na usalama wilayani Kakonko Mkoani Kigoma inawashikilia watu saba akiwemo Mwenyekiti na Mtendaji wa Kijiji cha Kikurazo na raia watano wa nchi ya Burundi  kwa kosa la kuwakodisha raia wa Burundi mashamba yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 100 ambayo ni mali ya kijiji hicho.


Akizungumza mara baada ya oparesheni iliyofanywa na kamati ya ulinzi na usalama katika kijiji hicho ikiwa ni pamoja na kukagua usalama wa mipaka ya Tanzania ,Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala alisema aliagiza kukamatwa kwa watu hao baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi wapenda maendeleo kuwa kuna baadhi ya wananchi kutoka Burundi katika eneo la Kumuka wamekodishiwa maeneo hayo na kulima mihogo, mahindi na karanga wakati baadhi ya wananchi wanakosa maeneo ya kulima.

Mkuu huyo walikuta kuna mshamba zaidi ya hekari 100 zinazolimwa na Warundi kwa kukodishiwa na viongozi wa kijiji kwa shilingi 40,000=/ hadi 60,000/= kwa hekari moja ili kujipatia fedha hizo ndipo walipomkamata mwenyekiti wa kijiji na mtendaji pamoja ma baadhi ya Warundi waliokuwa katika mashamba hayo.

Alisema wanaendelea kufanyiwa mahojiano na jeshi la polisi na watawafikishwa mahakamani.

"Tulifika mpakani kuangalia usalama wa mpaka wetu na tumekuta mpaka uko salama na tumefanya oparesheni na kubaini warundi wanalima kwenye ardhi yetu na baada ya mahojiano wamekili kabisa wanalima na wamekodishiwa na viongozi nipende kuwaambia Warundi na viongozi wa vijiji wasiifanye Tanzania kama shamba la bibi",alieleza.

 "Wananchi wetu na wao wanahitaji kulima na tutahakikisha hakuna Mrundi yeyote atakayevuna mazao hayo na tutahakikisha mazao hayo yanavunwa na wananchi wetu hatuko tayari kuona nchi yetu inaingia uhasama na nchi jirani kwa sababu ya baadhi ya viongozi wasio waaminifu", alisema Kanali Ndagala.

Aidha aliwataka viongozi na wananchi wa mipakani kuacha tabia ya kuwakodishia wananchi wa Burundi mashamba kwa kuwa ni kosa kisheria na kwa watakaobainika watafikishwa mahakamani.

Alisema oparesheni hiyo ni muendelezo wa oparesheni zingine kwa kuwa suala hilo linaweza kusababisha uvunjifu wa amani kutokana na miingiliano huo wa mipaka na kusababisha mipaka ya nchi kuibiwa na wageni.

Mtendaji wa kijiji cha Kikurazo Merikiadesi Evarist alikiri kuwa ni kweli maeneo hayo yamevamiwa na Warundi na baadhi ya wananchi hawana maeneo ya kulimia na yeye kama mtendaji wa kijiji hajahusika na suala hilo na yeye ameaminiwa kuwa mtendaji wa kijiji hicho kwa muda wa miezi sita iliyopita hivyo hakuwa anafahamu chochote kinachoendelea katika maeneo hayo.


Mwenyekiti wa Kijiji Enosi Rwanika  alisema Mwaka 2017 waliweka utaratibu wa kuhakikisha wananchi wanagawiwa maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo, baadhi walichukua na wengine hawakuweza kujitokeza ambao hawakujitokeza ndiyo hao wanaolalamika hawana maeneo ya kufanyia kilimo na waliochukua baaadhi yao wanawakodishia Warundi mashamba.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akikagua mpaka wa jiwe kati ya nchi ya Burundi na Tanzania katika Kijiji cha Kikurazo - Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527