Video : MTOTO WA MIAKA MITANO AMBURUZA POLISI BABA YAKE

AMA kweli kuishi kwingi kuona mengi: Hivi ndivyo unaweza kusimulia mkasa wa mtoto anayekadiriwa kuwa na miaka mitano alivyomfikisha baba yake mzazi kituo cha polisi huko Ngara mkoani Kagera.

Kisa chenyewe ni baada ya mtoto huyo kudai kubaini njama za baba yake kutaka kuuza shamba bila kuishirikisha familia yake hali ambayo ilimghadhabisha mtoto huyo na kwenda kumshitaki.

Picha ya video fupi iliyorekodiwa kwa njia ya simu juu ya mkasa huo ilizagaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuibua mjadala miongoni mwa makundi ya WhatsApp, Facebook na Instagram.

Sababu iliyowashtua na kuwavutia watu wengi ni umri wake unaokadiriwa kuwa miaka mitano na uwezo wake wa kupambanua mambo hadi kuchukua hatua ya kumshtaki baba yake ili kumzuia asiuze shamba lao.

Mtoto huyo alieleza namna alivyochukizwa na kitendo cha baba yake kutaka kuuza shamba.


"Anataka kuuza shamba sasa tutaishi wapi?" Anahoji mtoto huyo na kusema kuwa alimkuta baba yake akiandikishana na mteja na ndipo alipochukua uamuzi wa kwenda kumshtaki polisi.

Alieleza kuwa alitoka nyumbani kwao kijiji cha Kabanga wilayani Ng'ara mkoani Kagera hadi Polisi kwa kupanda lifti ya mtu aliyemtaja kwa jina la Thabiti.

Mtoto huyo ambaye alionekana kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa kwa kujiamini, alisema alipowaeleza kuhusu mkasa huo polisi walirudi naye hadi nyumbani na kuzuia mauziano hayo.

"Polisi walikuja wakamuuliza baba kama kweli anataka kuuza shamba, baba akasema hajauza...wakataka kumpeleka kituoni, nikakataa...," anaeleza zaidi.

Tazama video hapa chini jinsi mtoto huyo aliyekuwa akijieleza kutokana na maswali aliyokuwa akiulizwa njiani, alijieleza zaidi kuwa hana mama na anaishi na baba yake huyo peke yao.


Chanzo - NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527