Picha : DC SHINYANGA AFANYA ZIARA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO SHINYANGA VIJIJINI

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya maji katika kijiji cha Nyida na Mendo pamoja na mradi wa umwagiliaji maji (Skimu), kwenye mashamba ya mpunga katika kata ya Nyida katik halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Vijijini). 

Matiro amefanya ziara hiyo Februari 8,2018 na alianza ziara yake katika kijiji cha Nyida kwa kukagua mradi wa umwagiliaji maji (Skimu), kwenye mashamba ya mpunga yenye ukubwa hekta 421 sawa na hekali 1052.5 na kuwataka wakulima hao, kilimo chao kiwe na tija kwa kufanikiwa kuinuka kiuchumi pamoja na kubadilisha makazi yao kwa kuondoa nyumba za tope.

Alisema kilimo hicho cha umwagiiaji kwao ni moja ya faida walionayo na kuwataka kulima angalau mara mbili kwa msimu mmoja pamoja na kufuata ulimaji wa kisasa ambao utawapatia mavuno mengi na hatimaye kuinuka kiuchumi.

“Nataka kuona kilimo hiki cha umwagiliaji kinakuwa na tija kwenye maisha yenu ambapo kwenye kipindi cha mavuno nitakuja kuona maendeleo yenu ya kimaisha kwa kujenga nyumba za kisasa, na siyo kuongeza idadi ya wanawake jambo ambalo litawafanya kuendelea kuwa maskini,”alisema Matiro.

Aliongeza kuwa kilimo hicho kikiwa na faida kwao kitawafanya hata wafadhili wa mradi huo kutoka (JICA) kuvutiwa na kuongeza miradi ya namna hiyo kwenye maeneo mengine na kuwafanya wakulima kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua ambacho hakina uhakika wa kupata mavuno.

Mhandisi wa umwagiliaji kutoka ofisi ya halmshauri ya wilaya ya Shinyanga vijijini Godfrey Mbwambo,alisema mradi huo ulianza kujengwa kuanzia mwezi Agosti hadi Septemba mwaka 2017, kutoka kwa ufadhili wa shirika la JICA na kugharimu kiasi cha Shilingi milioni 100.

Akiwa katika kijiji cha Mendo Kata ya Ilola ,mkuu wa wilaya alikagua mradi wa maji ya kisima kirefu kwa kutekeleza ziara ya maagizo ya Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso na kukuta mradi huo bado haujafanyiwa marekebisho kwani mabomba yake bado yanavuja na kuagiza mkandarasi wa maradi huo afike ofisini kwake.

Matiro alieleza kukerwa na  mhandisi wa maji katika halmashauri hiyo Silvester Mpemba  kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kushindwa kusimamia wakandarsi hao wa miradi ya maji, na kusababisha kutekeleza ovyo miradi hiyo ambayo imekuwa haina tija kwa wananchi na kuendelea kutumia maji machafu.

Aidha alimtaka mhandisi huyo kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kukaa tu ofisini bali atembelee miradi yote ya maji inayotekelezwa kwenye halmashauri hiyo kwa kufanya ukaguzi na siyo kusubiri hadi ziara za viongozi ndipo naye afike kwenye miradi hiyo.

Hata hivyo mhandisi huyo alijitetea kuwa alishindwa kwenda kuukagua mradi huo kutokana na kukosa mafuta kwenye gari,na hivyo kukwama kabisa kuutembelea mradi huo, ambapo alikuwa akiwasiliana na mkandarasi kwa njia ya simu na kumweleza kila kitu kina kwenda vizuri na hatimaye kukuta madudu.

Akiwa katika kata ya Didia mkuu huyo wa wilaya aliivunja kamati ya maji kutokana na kufanya ubadhirifu kwenye mradi huo,kwa kutafuna pesa na kuufanya kushindwa kuendelea kuhudumia wananchi mara baada ya kifaa kimoja kuharibika na kukosekana pesa za matengenezo shilingi milioni 3.7 na kuufanya mradi kutaka kufa.

“Kamati hii kuanzia sasa nimeivunja na ninaagiza Sungusungu watu hawa watafutwe wakamate na wapelekwe Polisi sababu ni wahujumu uchumi, na kisha wapewe muda wa kizirudisha pesa zote walizozitafuna kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria,” alisema Matiro.Soma zaidi hapa <<Dc Shinyanga avunja kamati ya maji Didia>>

Matiro pia alikagua ujenzi wa miundo mbinu ya Zahanati ya Samuye ikiwemo maabara na nyumba ya watumishi sambamba na
kukagua ujenzi maabara na shimo la kuchomea uchafu katika kituo cha afya cha Tinde.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro (mwenye nguo nyekundu) akizungumza wakati akikagua mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa zao la Mpunga kwenye kijiji cha Nyida kata ya Nyida na kuwataka wakulima kilimo hicho kiwe na tija kwao kwa kuwanyanyua kiuchumi - Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog
Mhandisi wa umwagiliaji kutoka halmashuri ya Shinyanga vijijini Godfrey Mbwambo akimuelezea mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro jinsi mradi huo unavyonufaisha wakulima wa mpunga kwenye kijiji hicho cha Nyida ambapo pia wanatarajia kujenga bwawa litakalokuwa chanzo cha uhakika cha maji kwenye mradi huo na kutoutegemea mtot Tungu na Manonga.
Mmoja wa wakulima wa mpunga katika eneo hilo Luhende Malija ambaye amelima hekali 10 za mpunga kwenye mradi huo, akimuelezea Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro namna wanavyo pata Maji mengi kwenye mashamba yao na kutarajia kupata mavuno mengi.Alisema kilimo hicho cha umwagiliaji kimekuwa na faida kwao ambapo wamekuwa wakipata maji mengi na kutarajia kupata mavuno bila ya kuwa na wasiwasi.
 Skimu ya maji jinsi inavyopeleka maji kwenye mashamba ya mpunga Nyida
Muonekano wa la hekta 421 lililolimwa mpunga kwa njia ya umwagiliaji.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mendo John Kabodo akimuelezea Mkuu wa wilaya Josephine Matiro jinsi mradi huo ulivyokikwazo kwao ambapo pale unaoofunguliwa maji umekuwa ukipasua mabomba na haujawahi kufanya kazi tangu mwaka 2014 na umegharimu shilingi milioni 300.19 na unajengwa chini ya mkandarasi Zuberi wa mjini Shinyanga
Katikati ni mhandisi wa maji wa halmshauri ya Shinyanga Silivester Mpemba akijitetea kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kuwa alishindwa kufika kufanya ukaguzi kwenye mradi huo kutokana na kukosa mafuta kwenye gari na amekuwa akiwasiliana na mkandarasi kwa njia ya simu
Mkuu w wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza kwenye mradi wa maji Kijiji cha Mendo na kuonyesha masikitiko mradi huo bado kuna matatizo kutokana na mhandisi wa maji wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Silivester Mpemba kushindwa kufanya ukaguzi na kuufanya kuendelea kuwa mbovu, ambapo alikasirika na kuamua kuondoka eneo la mradi na kuwataka wakandarasi wote kufika ofisini kwake.
Mafundi wakiunganisha mabomba ambayo yamekuwa yakipasuka kwenye mradi huo wa maji Mendo
Mkuu wa wilaya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa kata ya Didia Shinyanga vijijini na kuivunja kamati ya maji kutokana na kufanya ubadhirifu wa fedha na kukwamisha mradi huo kutofanya kazi tena.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya maji iliyovunjwa Selemani Msabaha ,akizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na wananchi na kukiri mradi huo wa maji Didia umeshidwa kuendelea kutoa huduma baada ya fedha za matengenezo kukosekana shilingi milioni 3.7
Mkaguzi wa ndani wa halmashuri ya Shinyanga Sumbukeni Malela akieleza jinsi ubadhirifu wa fedha ulivyotumika kwenye mradi huo wa maji Didia ambapo kamati hiyo ilikuwa ikitoa fedha za matumizi na hapakuwepo na vikao halali huku fedha zingine shilingi 984,600 hazijulikani zilipo pamoja na mchanganuo wa fedha shilingi milioni 17 za makusanyo ya maji kutokuwa sahihi wala risiti za manunuzi hazipo
Afisa mtendaji wa kijiji cha Didia Ginai Lubacha akisoma taarifa kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na kueleza changamoto wanayokumbana nayo kwenye kijiji hicho kuwa ni kutokamilika kwa ujenzi wa kituo cha afya na kupongeza kukamilika kwa kituo cha polisi ambacho kitaimarisha ulinzi katika maeneo hayo
Diwani wa kata ya Didia Luhende Masele akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara na kuipongeza serikali kwa kukalimisha ujenzi wa kituo cha polisi eneo hilo na kupeleka askari kuanza kufanya kazi jambo ambalo litasaidia kupunguza matukio ya uhalifu katika eneo hilo
Mkurugenzi wa halmashuri ya Shinyanga  Bakari Kasinyo akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara Didia na kueleza kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha (2018-19) halmashuri imetengaShilingi Milioni 40 ambazo zitasaidia kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha afya
Mkurugenzi wa halmashuri ya Shinyanga  Bakari Kasinyo akizungumza katika mkutano wa hadhara Didia
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwataka vijana na akina mama kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali ili waweze kupata mikopo kwenye halmashauri asilimia 10 ambayo itawainua kiuchumi
Wananchi wa kata ya Didia wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro.

Wananchi wakimsikiliza mkuu wa wilaya
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akikagua ujenzi wa miundo mbinu ya zahanati ya Samuye ikiwemo ujenzi wa maabara na nyumba ya watumishi
Mafundi ujenzi wakimwagilia msingi wa jengo la maabara katika zahanati ya Samuye
Mkuu wa wilaya Shinyanga Josephine Matiro akiangalia ramani ya ujenzi wa maabara katika zahanati ya Samuye
Mkuu wa wilaya Shinyanga Josephine Matiro akiwa katika eneo la ujenzi wa majengo mbalimbali katika kituo cha afya Tinde
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga akikagua ujenzi maabara na shimo la kuchomea uchafu katika kituo cha afya cha Tinde.
Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527