DC MATIRO AVUNJA KAMATI YA MAJI KATA YA DIDIA KWA UBADHIRIFU WA FEDHA


Mkuu wa wilaya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa Kata ya Didia Shinyanga na kuivunja kamati ya maji kutokana na kufanya ubadhirifu wa fedha na kukwamisha mradi huo kutofanya kazi tena. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog
Wananchi wa kata ya Didia wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro.
Aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya maji iliyovunjwa kata ya Didia Selemani Msabaha akizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro na wananchi na kukiri mradi huo wa maji Didia kuwa umeshidwa kuendelea kutoa huduma mara baada ya fedha za matengenezo Shilingi milioni 3.7 kukosekana 
Mkaguzi wa ndani wa halmashuri ya Shinyanga vijijini Sumbukeni Malela ,akieleza jinsi ubadhirifu wa fedha ulivyotumika kwenye mradi huo wa maji Didia.Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

*****
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ameivunja Kamati ya maji ya kata ya Didia iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kutokana na kufanya ubadhirifu kwenye mradi wa maji wa kisima kirefu.

Kamati hiyo inadaiwa kutafuna pesa za mradi ulioanza kujengwa mwaka 2013/2014 na kukabidhiwa mwaka 2016 na kugharimu shilingi milioni 400.16 umeshindwa kuendelea kuhudumia wananchi mara baada ya kifaa kimoja kuharibika na kukosekana pesa za matengezo na kuufanya mradi kutaka kufa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Didia jana Februari 8,2018 mkuu wa wilaya aliamua kuvunja kamati hiyo na kuagiza wajumbe wa kamati hiyo wakamatwe.

“Kamati hii kuanzia sasa nimeivunja na ninaagiza jeshi la jadi Sungusungu watu hawa watafutwe wakamate na wapelekwe Polisi sababu ni wahujumu uchumi na kisha wapewe muda wa kizirudisha pesa zote walizozitafuna kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria,” alisema Matiro.

Hata hivyo mara baada ya kuivunja kamati hiyo ya maji, alisimamia zoezi la wananchi kuchagua viongozi wengine sita wa mpito kupitia mkutano huo wa hadhara kwa kuchaguliwa na wananchi wakiongozwa na mwenyekiti wake Katunge Njile, huku akiagiza viongozi wote wa vitongoji kuitisha mikutano ya hadhara na kuchagua wajumbe wawili wawili ambao wataunda kamati ya maji ya kudumu.

Pia aliagiza kila kaya kwenye kata hiyo ya Didia yenye wakazi 4112 wachange shilingi 3000, fedha ambazo zitasaidia kununua kifaa kwenye mradi huo wa maji chenye gharama ya shilingi milioni 3.7, ili uanze kufanya kazi na kuondoa adha ya wananchi kutumia maji machafu sambamba na kumtua ndoo kichwani mwanamke.

Naye aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo ya maji Selemani Msabaha, alikiri kuwa walishindwa kuendesha mradi huo mara baada ya pesa kukosekana ambapo mpaka sasa kwenye akaunti kuna shilingi 129,000.

Kwa mujibu wa mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo Sumbukeni Malela kamati hiyo ilikuwa ikikusanya hadi shilingi milioni 17 na walikuwa hawafanyi vikao na hakuna listi za manunuzi ya vifaa vinapoharibika na kwamba kiasi cha shilingi 984,600 hazijulikani zilipo.

Na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527