DC GAGUTI AKUTANA NA WAZEE WA BUHIGWE..AHAMASISHA USHIRIKIANO SHUGHULI ZA MAENDELEO

Mkuu wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Kanali Marco Gaguti amewataka watendaji wa serikali pamoja na wananchi kushirikiana katika shughuli za maendeleo katika ukusanyaji wa mapato na kufanya kazi ili kuboresha huduma za kijamii katika wilaya hiyo na kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Wito huo aliutoa juzi katika chakula cha pamoja na wazee wa wilaya ya Buhigwe ,watumishi wa serikali, viongozi wa dini na chama wilayani humo pamoja na kuhamasisha shughuli za maendeleo akiwataka kila mwananchi mmoja mmoja, kwa makundi na kwa ujumla wao kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu, afya, miundombinu na jinsi ya kupatikana haki za wazee.

Mkuu huyo aliwataka watendaji wa halmashauri kwa kushirikiana na wananchi wote ndani ya wilaya kusaidia jitihada za kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa mafanikio makubwa ambapo mapato hayo yatasaidia vijiji ambavyo havina zahanati vipate huduma hiyo kutokana na mapato hayo.

Aidha Gaguti aliwataka watendaji wa serikali kuhakikisha wazee wa wilaya hiyo wanapata haki zao kama wengine ikiwa ni pamoja na kupatiwa matibabu bure, kwa kuwa ni sera ya taifa mzee asisumbuliwe na apatiwe huduma zote bila malipo.

“Nawashukuru sana wazee, viongozi wa vya siasa, viongozi wa madhehebu ya dini pamoja na watumishi wote kwa kuonyesha moyo wa kusimamia maendeleo yetu na kuhakikisha tunapata maendeleo kwa kasi ni imani yangu kuwa tutashilikiana kwa mambo mengi ili kuweza kuinua uchumi wetu", alisema Gaguti.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe Anosta Nyamoga alieleza kuwa Halmashauri ya Buhigwe inatoa huduma za afya kwa wazee katika vituo vyake vya kutolea huduma za afya bure kulingana na sera na miongozo ya serikali.

"Wazee wanapewa kipaumbele katika matibabu kwa kutibiwa kwanza ,wazee 14,993 wametambuliwa katika wilaya yetu na wazee 1000 watapigwa picha na kupewa vitambulisho vya matibabu katika kata 5, Upigaji wa picha na utoaji wa vitambulisho utaendelea katika kata 15 ambazo bado hazijafikiwa, Halmashauri imeendelea kuhamasisha jamii ili kuona umuhimu wa kujiunga na mfuko wa afya wa jamii (CHF)",alisema.

Nao baadhi ya wazee wa wilaya ya Buhigwe, Loleye Ndalibhonye alimpongeza mkuu wa wilaya kwa kuwakumbuka na kuwasaidia katika huduma za kijamii na kuwasaidia katika kuwapatia huduma ya afya bure.

Alisema endapo wilaya hiyo ikiongeza vituo vya Afya itasaidia wazee hao kupata huduma kwa urahisi na wananchi kuweza kupata huduma hiyo na kupunguza vifo vitokanavyo na ukosefu wa huduma.
Na Rhoda Ezekiel- Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Kanali Marco Gaguti akizungumza na wazee wa wilaya ya Buhigwe ,watumishi wa serikali, viongozi wa dini na chama tawala.
Mmoja wa wazee hao akizungumza
Mkuu wa wilaya akiwa katika picha ya pamoja na wananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527