MBINU ZA KUKABILI UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME


UPUNGUFU wa nguvu za kiume ni hali ya kiungo cha uzazi cha mwanaume (uume) kutokuwa na nguvu ya kutosha kufanikisha tendo la ndoa kama vile kushindwa kuanza au kukamilisha tendo lenyewe.

Karibu kila mwanaume ambaye yupo kwenye mahusiano amewahi kupata tatizo hili angalau mara moja. Hali hii ni ya kawaida kama inatokea mara chache, lakini kama inajitokeza mara kwa mara ni muhimu kupata ushauri wa kitaalamu.

Vilevile nguvu za kiume huanza kupungua kuanzia umri wa miaka 50. Mabadiliko haya ni ya kawaida, hayahusiani na tatizo lolote la kiafya endapo hayasababishi kushindwa kabisa tendo la ndoa.

Ili uume uweze kuwa na nguvu ya kufanikisha tendo la ndoa ni lazima damu iende kwenye mishipa ya uume kwa kiwango cha kutosha na iweze kubaki sehemu hiyo kwa muda mrefu.

Sehemu mbalimbali za mwili zinafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha mfumo huu mzima unafanya kazi sawasawa ikiwa ni pamoja na mishipa ya damu na fahamu, ubongo pamoja na vichocheo vya mwili (hormones).

Hali yoyote ya mwili inayosababisha damu kushindwa kufika kwenye mishipa ya uume au kutokaa muda wa kutosha, na hitilafu katika mfumo wa neva kati ya uume na ubongo inaweza kuleta upungufu wa nguvu za kiume.

Vile vile saikolojia ina sehemu kubwa katika kufanikisha tendo la ndoa. Sababu za kupungua kwa nguvu za kiume zimegawanyika katika makundi makuu mawili; sababu za kiafya na sababu za kisaikolojia.

Matatizo ya kiafya ambayo yanasababisha upungufu wa nguvu za kiume ni magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo la juu la damu; uzito mkubwa; na baadhi ya dawa. Mfumo wa maisha unaoongeza uwezekano wa kupunguza nguvu za kiume ni unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji sigara.

Sababu za kisaikolojia ni pamoja na hali ya wasiwasi, msongo wa mawazo au kutokuwa na maelewano na mwenza wako. Mara nyingi sababu za kiafya na kisaikolojia hutokea kwa pamoja na zinategemeana; hasa kwa sababu kukosekana kwa nguvu za kiume kunaleta athari za saikolojia; athari za kisaikolojia zinaleta upungufu wa nguvu za kiume; hivyo kunakuwa na mzunguko wa tatizo.

Dalili kuu ya upungufu wa nguvu za kiume ni uume kutokuwa na nguvu ya kutosha kuanza tendo la ndoa au nguvu kuisha kabla ya kukamilisha tendo. Kupungua kwa nguvu za kiume kwa sababu za kiafya kunaweza kutofautishwa na sababu za kisaikolojia kwa kuangalia iwapo kupungua huku ni kwa mfululizo au hutokea kwa nyakati fulani tu.

Endapo tatizo linatokea kwa nyakati maalumu tu kwa mfano wakati umebadilisha mwenza, uwezekano mkubwa ni tatizo la kisaikolojia. Lakini kama tatizo ni la muendelezo na linaongezeka ukubwa siku hadi siku, inawezekana kuna tatizo la kiafya.

Mtaalamu wa afya anaweza kupambanua na kufanya vipimo vinavyostahili ili kuweza kubaini chanzo cha tatizo. Mara nyingi watu wameshindwa kutafuta ushauri wa kitaalamu kwa wakati, kwa sababu ya kuona kuwa suala hili ni la usiri na wasingependa kuliongelea; hata hivyo ni muhimu kupata ushauri ili kubaini chanzo na kuweza kupata msaada wa kitaalamu mapema.

Madhara yatokanayo na upungufu wa guvu za kiume yanaonekana zaidi katika saikolojia ambapo muathirika anapata msongo wa mawazo na wasiwasi; vilevile husababisha mafarakano kwenye mahusiano.

Na endapo tatizo ni kubwa linaweza kuleta ugumba. Matibabu ya upungufu wa nguvu za kiume yanategemea na chanzo cha tatizo. Iwapo chanzo kitagundulika mfano kama ni dawa za ugonjwa fulani, daktari anaweza kushauri kubadilisha aina ya dawa; na ikiwa tatizo lipo kwenye upungufu wa vichocheo vya kiume daktari anaweza kushauri kutumia dawa za kuongeza vichocheo hivyo mwilini.

Vilevile zipo dawa zinazotumika kuongeza msukumo wa damu kwenye uume na hizi zinatumika ili kuongeza nguvu za kiume. Japokuwa dawa hizi zinauzwa kwenye maduka ya dawa, ni vizuri kupata ushauri wa daktari kabla ya kuzitumia ili kuweza kubaini chanzo, na endapo unastahili kutumia dawa hizo au la.

Njia za kupunguza uwezekano wa kupata tatizo la kupungua kwa nguvu za kiume ni kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi, kupunguza unywaji wa pombe na kuacha kuvuta sigara.

Vilevile ni muhimu kupata ushauri wa kitaalamu iwapo unasumbuliwa na msongo wa mawazo au tatizo lolote la kisaikolojia. Uchunguzi wa afya mara kwa mara utabainisha magonjwa kama vile kisukari na shinikizo la damu na kuyadhibiti mapema kabla hayajaleta athari za kupungua kwa nguvu za kiume.

Faraja Chiwanga ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Tiba na Mbobezi wa magonjwa ya Homoni. Simu: 0786587900

Chanzo- Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527