MTOTO WA MIAKA 8 ACHOMWA MOTO BAADA YA KUIBA SHILINGI ELFU 5 SHINYANGA



Mkono wa mtoto aliyechomwa moto
***
Mkazi wa Kijiji cha Azimio Kata ya Salawe, Felister Mdoshi amemchoma moto mjukuu wake kwa kutumia mfuko wa nailoni aliomfunga mkononi, akimtuhumu kumuibia Sh5,000.

Licha ya kumfanyia ukatili huo mjukuu wake anayejulikana kwa jina la Elizabeth Mussa (8), mwanafunzi wa darasa la awali Shule ya Msingi Azimio, bibi huyo aliamua kumfungia ndani kwa muda wa siku 11 bila kumpatia matibabu tangu kufanyika kwa tukio hilo Agosti 13 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Azimio Twiga Mashimba alisema juzi kuwa alichomwa moto Agosti 13, 2017 lakini tukio hilo limegundulika Agosti 24,2017 baada ya majirani kutoa taarifa juu ya kitendo hicho baada ya kubaini kilichofanyika dhidi ya mtoto huyo.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga, Simon Haule alipotafutwa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo, alisema yuko kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga hivyo hataweza kulizungumzia tukio hilo kutokana na mazingira alipo.

“Tukio hili linasikitisha mtoto huyu kafanyiwa kitendo cha kikatili na bibi yake na sisi tulipopata taarifa tulienda hadi nyumbani kwa bibi huyo na kweli tulimkuta mtoto ana hali mbaya, tulipomhoji kwanini kafanya kitendo hicho alikiri na kudai ana mazoea ya kuiba fedha zake mara kwa mara ndiyo maana kamchoma moto,” alisema.

Mganga Mfawidhi Msaidizi Kituo cha Afya, Salawe Anastazia alikiri kumpokea mtoto huyo akiwa na majeraha makubwa yaliyotokana na kuungua na moto, ambapo alibainisha kuwa hali yake siyo nzuri kutokana na vidonda kuanza kuoza.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Yunis Mazige ambaye alikuwa akiishi mbali na mtoto wake kutokana na kuolewa na mwanamume mwingine, alisema hana chakumfanya kwasababu kitendo hicho kimefanywa na mama yake mzazi kwani alimuamini na kumpa mtoto wake na walikuwa wakiishi vizuri kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano.

Diwani wa Kata ya Salawe, Joseph Buyugu licha ya kulaani kitendo hicho, pia alisema tayari mwanamke huyo anashikiliwa na jeshi la polisi.
Habari imeandaliwa na Waandishi wa Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527