RUSHWA KWENYE VYOMBO VYA KUTOA HAKI YATAJWA KUWA KIKWAZO KIKUBWA UPATIKANAJI WA HAKI ZA WATOTO

Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO,Gelard Ng’ong’a.
*****
Wadau wa haki za mtoto na ulinzi wa mtoto wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wameeleza kuwa jitihada za kumlinda mtoto zinakwama kutokana na maeneo mengi yanayotoa haki ikiwemo polisi na mahakama kugubikwa na vitendo vya rushwa kutokana na baadhi ya watumishi kutokuwa waaminifu na kutozingatia maadili ya kazi zao. 

Wakizungumza jana mjini Kahama katika kikao cha kutambulisha mradi wa "Mradi wa ulinzi wa mtoto,haki za mtoto na utawala" unaotekelezwa na Shirika la Rafiki SDO kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la kuhudumia watoto “Save The Children International” kwa hisani ya shirika la Maendeleo la nchini Sweeden – SIDA. 

Akichangia mada hiyo ya namna bora ya kumlinda mtoto, Diwani wa kata ya Kagongwa Hamis Kashantole alisema tatizo kubwa ni watu waliopewa dhamana ya kutoa haki kuendelea kuwakandamiza watoto.

Alisema ipo haja ya kuona namna bora ya kutoa elimu kwa watoa maamuzi kama mahakama ili wapunguze mlolongo wa kutoa haki kwa watoto jambo litakalosaidia watoto kupata haki zao.

Nao watoto walioshiriki kikao hicho walisema watoto wengi wamekuwa wakibakwa, kunyanyaswa na watu au wazazi lakini bado haki zao zimekuwa hazipatiwi nafasi katika kuzijadili.

Hata hivyo, mgeni rasmi katika zoezi la kutambulisha mradi huo kwa upande wa mji wa Kahama, diwani wa kata ya Kahama mjini Hamidu Juma alisema ikiwa elimu itatolewa ipasavyo katika ulinzi wa mtoto, haki zao zitapatikana.

Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO,Gelard Ng’ong’a mradi huo unalenga kumlinda mtoto na kuhakikisha watoto wanapata haki zao pamoja na kuwajengea uwezo wa kupaza sauti zao ili kuhoji haki hizo kutoka kwa wazazi, viongozi na wadau wengine wanaohusika. 

Alieleza kuwa katika Mji wa Kahama mradi huo utatekelezwa kwenye kata ya Mwendakulima, Nyihogo, Kagongwa, Nyasubi, Majengo, Kahama mjini, Mhongolo Zungomela, Nyandekwa na Busoka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post