SERENGETI BOYS KUMENYANA NA MALI MICHUANO YA AFCON NCHINI GABON LEO

Hatimaye siku iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu na Watanzania ya kuishuhudia timu yao ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imefika ambapo, leo Jumatatu inafungua pazia lake katika mashindano ya Kombe la Afrika kwa Vijana, kwa kumenyana na Mali katika michuano hiyo inayofanyika nchini Gabon.

Aidha, Serengeti Boys imepangwa katika Kundi B, ambapo katika kundi hilo iko pamoja na timu nyingine za Angola na Niger ambazo nazo zitakuwa kibaruani leo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime amesema kuwa kikosi cha Serengeti Boys kiko vizuri na kimejiandaa vya kutosha kuwakabili vijana wa mali kwenye mchezo huo wa kwanza.

“Kikosi kipo vizuri na tumejipanga kuikabili vilivyo timu ya Mali kwani tunataka kuwafurahisha Watanzania kwa kutowaangusha na naomba wazidi kutuombea,” amesema Bakari Shime.

Timu hiyo ya Taifa ya vijana pamoja na maandalizi mazuri lakini imepata pigo baada ya nahodha, Abd Makamba kuvunjika mguu hivyo hataweza kushiriki mashindano yote.

"Ni jambo la kusikitisha kidogo kwamba Nahodha wetu Issa Abdi Makamba alipata mpasuko wa mguu juzi mazoezini kwa bahati mbaya akiwa pekee yake kabisa…Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa madaktari wangu wamesema kwamba hatoweza kushiriki mashindano haya na jina lake tumeliondoa katika mashindano tayari nafasi yake imeshachukuliwa na mtu mwingine kwa sababu tulikuwa na wachezaji wa akiba". Alisema Shime na kuongeza;
 
“Imekuwa bahati mbaya kwetu, bahati mbaya kwa Issa Abdi amepambana kwa miaka miwili kuiongoza hii timu kuhakikisha inafikia hapa ambapo imefika lakini tunaamini mchango wake ni mkubwa sana na kwa sababu bado yupo ndani ya kikosi anaendelea na majukumu yake kama Kapteni kuhamasisha na kuongoza wenzake bado tunampa pole Issa Abdi tunaamini kabisa wachezaji wanatakiwa kupigana kwaajili yake”.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527