MAPYA YAIBUKA KIFO CHA KATIBU WA CCM, WAUAJI WALIACHA UJUMBE 'MAREHEMU ALIKUWA ANADHULUMU WATU'

Siku moja baada ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Bungu wilayani Kibiti, Alife Mtulia, kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake, imeelezwa kuwa wauaji hao waliacha ujumbe wakidai marehemu alikuwa akidhulumu watu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema mauaji hayo yalifanyika usiku wa kuamkia jana, huku akiahidi kutoa ufafanuzi wa kina leo.

Mauaji ya askari Polisi, viongozi wa Serikali za Mitaa na raia yamekuwa yakifanyika mara kwa mara katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani.

“Mtulia aliuawa akiwa anaelekea bafuni kuoga. Walimvamia wakampiga risasi na kupoteza maisha. Hili tukio limetokea kweli ameuawa. Ila marehemu hakuwa  katibu wa chama wa tawi, alikuwa kiongozi miaka ya nyuma sielewi alistaafu lini,” alisema.

Alibainisha kuwa sababu za mauaji hayo hazijafahamiaka, licha ya wauaji hao kuacha ujumbe wa maandishi.

“Katika ujumbe huo wauaji walidai kuwa marehemu alikuwa mtu wa kudhulumu. Ila hawakusema alidhulumu lini na alimdhulumu nani,”alisema.

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa watu waliofanya mauaji hayo, mpaka jana jioni hakuna mtu aliyekamatwa.

“Tunaendelea na msako. Nawataka tu wananchi kuwa watulivu katika kipindi hichi ambacho tunaendelea kuwasaka wauaji,” alisema.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi liliwaua watu wanne wanaosadikiwa kuhusika na mauaji ya askari polisi wanane na uporaji wa silaha katika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani. Tukio hilo lililotokea takribani wiki mbili zilizopita.

Jeshi hilo lilieleza chanzo cha mauaji ya askari polisi kujirudia mara kwa mara katika maeneo hayo ya Mkuranga, Rufiji, Ikwiriri na Kibiti kuwa ni eneo hilo kuzungukwa na pori.

Akizungumza kuhusu tukio hilo katika Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya alisema baada ya majambazi hao kuwaua askari hao walipora bunduki saba na kutokomea kusikojulikana.

Alisema baada ya tukio hilo polisi walifanya operesheni na kufanikiwa kutambua maficho ya muda ambapo katika majibizano ya risasi walifanikiwa kuwaua watu hao wanne pamoja na kupata silaha nne mbili zikiwa ni za askari waliouawa na mbili za majambazi hao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527