Picha 31: MKUTANO MKUBWA KWENYE SHULE ILIYOKUMBWA NA MAPEPO SHINYANGA ...VIONGOZI WA DINI WASHUSHA UPAKO



Machi 29,2017 mtandao huu wa Malunde1 blog uliripoti kuhusu Shule ya sekondari Imesela kuvamiwa na mapepo na kuwafanya wanafunzi kuanguka na kutamka maneno yasiyoeleweka.

Hali hiyo ilimlazimisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama kufika shuleni hapo na kujionea hali halisi na kutangaza ufanyike mkutano siku ya Ijumaa Machi 31 kwa ajili kutafutaufumbuzi wa tatizo hilo.

Sasa leo Machi 31,2017,Viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Shinyanga wamefanya maombi maalum kuwaombea wanafunzi waliopatwa na mapepo na kusababisha kuanguka na kupiga kelele wakitamka maneno yasiyoeleweka katika shule ya sekondari Imesela iliyopo wilaya ya Shinyanga.

Viongozi hao wa dini walifika shuleni hapo wakiongozana na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga ikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Josephine Matiro.

Viongozi hao wa dini mara baada ya kufika katika shule hiyo walishuhudia wanafunzi wakianguka,kugaragara huku wakitamka maneno ya ajabu ajabu ambapo mwandishi mkuu wa Malunde1 blo,Kadama Malunde ameshuhudia viongozi hao wakiwafanyia maombi wanafunzi hao na kurudi katika hali zao za kawaida.

Viongozi hao wa dini pia walifanya maombi madarasani,vyoo vya wanafunzi na kwenye baadhi ya miti iliyopo katika shule hiyo ambapo baadhi inadaiwa kuwa pale inapoguswa watu hupigwa shoti kama ya umeme.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa maombi hayo mwenyekiti wa makanisa ya kipentekoste mkoa wa Shinyanga Mchungaji Elias Madoshi kutoka kanisa la FPCT alisema wamefika hapo kuvunja nguvu za shetani ambazo zinawafanya wanafunzi wakose masomo yao na kwamba jambo hilo ni la aibu na fedheha kubwa katika nchi.

“Sisi viongozi watumishi wa mungu tuliopewa mamlaka na mungu kabla hatujaja hapa tumeoneshwa na mungu tumeshamjua mhusika wa mchezo huu wa kijinga,tunamuonya na tunamtaka aache kuanzia sasa,kama hataacha mtamzika hapa kijijini,tunamtaka asirudie mungu hachezewi”,alisema mchungaji Madoshi. 

Naye Askofu Josephat Mussa wa kanisa la Tanzania Mision Revival Church (TMRC) alisema viongozi wa dini kamwe hawawezi kukaa kimya na kufurahia vitendo hivyo vya kishirikina na kwamba viongozi wa dini watafanya kambi katika kata ya Imesela ili watu wamjue mungu.

Kwa upande wake Kiongozi wa Jumuiya ya Waislamu Wahmadiyya mkoa wa Shinyanga (Ahmadiyya Muslim Jamaat Shinyanga),Sheikh  Shabani Luseza alishauri wananchi kumwamini mungu kwani kama huna ulinzi wa mwenyezi huna lazima vitendo vya mashetani,mizimu lazima vikupate.

“Lazima mmrudie mungu,asilimia 60 mpaka 70 ya watu Shinyanga hawafuati dini ndiyo maana matatizo haya yanajitokeza,ukiamua kumwelekea mungu naye atakuelekea na kukupa ulinzi”,aliongeza sheikh Luseza.

Sheikh Masoud Ramadhan kutoka Shinyanga mjini alieleza kukerwa na vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa wanafunzi hao na kuongeza kuwa kviongozi wa dini wamekubaliana kushirikiana ili kumaliza tatizo linalowakumba wanafunzi wa shule ya sekondari Imesela.

Awali kabla ya kufanya maombi hayo maalumu mkuu wa wilaya alifanya mkutano na wananchi wa kata ya Imesela na kata jirani kujadili namna ya kumaliza tatizo hilo ambapo kwa pamoja walikubaliana viongozi wa dini wafanye maombi badala ya kutumia njia za kienyeji (waganga) kumaliza tatizo hilo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema tatizo la wanafunzi kufanyiwa vitendo vya kishirikina linawaathiri wanafunzi na kusababisha kutohudhuria vipindi darasani kwa kukumbwa na mapepo hayo.

Aidha Matiro aliwataka wananchi kumwamini mungu kwa kila jambo badala ya kuamini katika matambiko kwani hakuna nguvu inayoweza kumshinda mwenyezi mungu.

Kufuatia maombi hayo wanafunzi wa shule hiyo walieleza kufarijika na hatua ya uongozi wa wilaya kufika na viongozi wa dini kufanya maombi hali ambayo inawapa matumaini ya kuendelea na masomo.

Wanafunzi wa shule ya sekondari Imesela yenye jumla ya wanafunzi 252 iliyoanzishwa mwaka 2006 wamekumbwa na mapepo yanayowaangusha na kujikuta wakitamka maneno yasiyoeleweka huku wakitaja majina ya wahusika wanaowafanyia ushirikina.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la shule hilo tatizo hilo limeanza mwezi Novemba mwaka 2016 na hali ilianza kuwashtua mwezi Januari mwaka 2017 na hali ilikuwa mbaya zaidi mwezi Machi mwaka huu ambapo wanafunzi 16 walipatwa na ugonjwa huo usiofahamika na hali imeendelea hivyo kila wanapofika tu shuleni saa moja na nusu asubuhi.


ANGALIA MATUKIO KATIKA PICHA YALIYOJIRI WAKATI WA MKUTANO NA MAOMBI KATIKA SHULE YA SEKONDARI IMESELA
Wananchi wa kata ya Imesela wakimsaidia mwanafunzi aliyepandisha mapepo wakati wa mkutano wa hadhara uliokusanya mamia ya wakazi wa kata ya Imesela na kata za jirani kujadili namna ya kumaliza tatizo la watoto kuanguka na kupiga kelele
Wananchi wakiwasaidia wanafunzi waliopandwa na mapepo
Wananchi wakiwa wamembeba mwanafunzi aliyepandisha mapepo
Mzazi akiwa amepandwa na hasira baada ya mtoto wake kupandisha mapepo shuleni...Inaelezwa kuwa mzazi huyo alianza kulia baada ya kupigwa ngumi na mtoto wake ambaye ni mwanafunzi katika shule ya sekondari Imesela aliyekuwa amepandisha mashetani/mapepo
Mwenyekiti wa kijiji cha Maskati kata ya Imesela Hamis Salum akifungua mkutano wa hadhara
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano huo ambapo aliwaomba watoe mawazo namna ya kumaliza tatizo lililojitokeza kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Imesela ambao wanapandisha mapepo kisha kuanza kuanguka,kupiga watu na kutamka maneno yasiyoeleweka
Wananchi wakiwa eneo la mkutano
Mkazi wa Imesela akichangia hoja namna ya kumaliza tatizo katika shule hiyo
Mkazi wa Imesela akichangia hoja kwenye mkutano
Mkazi wa Imesela akichangia hoja
Mkazi wa Imesela akizungumza wakati wa mkutano huo
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akisikiliza hoja za wananchi
Walimu wa shule ya sekondari Imesela wakiwa eneo la mkutano
Mwenyekiti wa makanisa ya kipentekoste mkoa wa Shinyanga mchungaji Elias Madoshi akizungumza wakati wa mkutano huo
Askofu Josephat Mussa wa kanisa la Tanzania Mision Revival Church (TMRC) akizungumza wakati wa mkutano huo
Kiongozi wa Jumuiya ya Waislamu Wahmadiyya mkoa wa Shinyanga (Ahmadiyya Muslim Jamaat Shinyanga),Sheikh  Shabani Luseza akizungumza katika shule ya sekondari Imesela
Sheikh Masoud Ramadhan kutoka Shinyanga mjini akieleza namna viongozi wa dini walivyokubaliana kufanya maombi katika shule ya sekondari Imesela
Viongozi wa dini wakijadili jambo kabla ya kuanza kufanya maombi katika shule ya sekondari Imesela
Wananchi wakiwasaidia wanafunzi waliopandwa na mapepo wakati wa mkutano huo
Viongozi wa dini wakiondoka kwenye mti mkubwa baada ya kumaliza kufanya maombi
Viongozi wa dini wakiendelea kufanya maombi eneo la shule ya sekondari Imesela
Maombi yanaendelea eneo la shule
Viongozi wa dini wakifanya maombi katika choo cha wanafunzi
Viongozi wa dini wakifanya maombi katika mti unaodaiwa kupiga shoti watu
Maombi yanaendelea katika mti mkubwa uliowekewa kengere katika shule ya sekondari Imesela
Wanafunzi katika shule ya sekondari Imesela wakiomba pamoja na watumishi wa mungu
Viongozi wa dini wakiendelea kuwaombea wanafunzi waliokumbwa na tatizo la kuanguka na kupoteza fahamu na kutamka maneno yasiyoeleweka
Maombi yanaendelea
Maombi yanaendelea katika shule ya sekondari Imesela
Mkuu wa wilaya Josephine Matiro akiwatia moyo wanafunzi wa shule ya sekondari Imesela kuendelea na masomo yao baada ya kufanyiwa maombi na viongozi wa dini

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Soma pia hii

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527