Mwanamme aliyejitambulisha kwa jina
la Shaban Charles(30) amejikuta katika wakati mgumu baada ya kushushiwa kipigo
na wananchi wa kitongoji cha Buyambelele Magharibi kijiji cha
Bugayambelele kata ya Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga wakimtuhumu
kuwaingilia wanawake nyakati za usiku kisha kufanya nao mapenzi kwa njia
za kishirikina.Anaripoti Kadama Malunde
Tukio hilo limetokea leo majira ya
saa kumi jioni ambapo wakazi wa kitongoji cha Bugayambelele Magharibi jirani na
kijiji cha Nhelegani kilichokumbwa na taharuki ya kuwepo mtu anayefanya mapenzi
na wanawake kimazingara.
Wananchi hao walimshtukia jamaa huyo
baada ya kuonekana akifanya vitendo walivyodai kuwa vya kishirikina katika familia
mbili za kitongoji hicho hali iliyosababisha wamhusishe moja kwa moja na tukio
lililozua gumzo katika kata hiyo la mtu asiyejulikana kufanya mapenzi na kuiba
mali za wananchi kishirikina.
Wakizungumza na Malunde1 blog wakazi
wa eneo hilo walisema mtu huyo aliingia kwenye nyumba mbili(kaya mbili ya
James Shilugu na Masele Shija) bila kupiga hodi huku akidai kuwa alikuwa
anatafuta mke wake,akidai kuwa ametoka kwa mganga wa kienyeji kaelekezwa kuwa
mke wake yupo eneo hilo amejificha.
Hata hivyo baada ya wananchi
kumtilia mashaka, jamaa huyo alianza kukimbia na kutupa simu zaidi ya tatu za
mkononi alizokuwa nazo wananchi wakafanikiwa kumkamata wakaanza kumpiga kisha
kumpeleka kwenye mkutano wa sungusungu na walipompekua wakamkuta na dawa za
kienyeji zinazodaiwa kuwa za mapenzi,zikisomeka kama ifuatavyo;
“Imala yose -kuchoma kuomba mke wako
roho yake ili irudi kwako aje kwako”na nyingine maandishi yakisomeka
"kuoga na kuchoma kuomba mkeo akupende na arudi kwako”.
Wakazi wa eneo waliendelea
kumshambulia mtu huyo kwa kutumia silaha za jadi ikiwemo fimbo na marungu kabla
ya askari wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kufika eneo la tukio kisha
kumpandisha kwenye gari na kuondoka naye.
Wakazi wa eneo hilo waliofikiwa na
mwanamme huyo Masele Shija na Francis Shilugu kutoka familia ya James Shilugu
na Masele Shija walisema vitendo alivyokuwa anafanya mwanamme huyo havikuwa vya
kawaida.
“ Huyu jamaa alifika hapa akakaa
kwenye zizi la ng’ombe,Kulikuwa na mtoto anacheza nje ya nyumba,tukamwambie
hebu muangalie huyo mtu anafanya nini hapo,akamuuliza kulikoni uko hapa,jamaa
akasema natafuta mke wangu amekuja kutafuta nyumba apange, akamuuliza unasema
kweli?,ndipo jamaa akachukua baiskeli yake aliyokuwa ameiweka kwenye minyaa
akaichukua na kukimbia ndipo akaibukia kwenye familia ya James
Shilugu”,alieleza Masele Shija.
“Alikuwa na baiskeli alipofika
karibu na nyumbani kwetu akailaza chini,ghafla nikamuona anaingia ndani baadaye
akatoka ndani ya nyumba yetu,nikamuuliza wewe nani na umeingiaje humu tena bila
hodi,akasema anatafuta mke wake ameingia ndani na mwanamme na amepotea
kimiujiza”,alisema.
“Nikaita majirani,tukampeleka kwenye
kengele(mkutano wa sungusungu),walipoanza kumuuliza maswali akaanza
kukimbia,wakamkimbiza wakamshika,alikuwa na simu akazitupa akabakiza moja
tu”,alieleza Francis Shilugu.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo Suzan
Stanslaus alisema kutokana na vitendo alivyokuwa anaonesha mwanamme huyo
kulikuwa na dalili za wanawake kuingiliwa kimwili kwa njia za kishirikina usiku
kwani wamekuwa wakisikia taarifa za wanawake kubakwa na wanaume kulazwa nje ya
nyumba katika kijiji jirani cha Nhelegani.
“Mimi nilikuwa nyumbani kwangu
wakaja wanakijiji wakiwa na mwanamme huyu wakidai ndiye amekuwa akiwafanyia
mchezo mchafu akina mama usiku na kuiba simu za watu,na leo alipokamatwa
alikuwa na simu nyingi na dawa za kienyeji”,alieleza Stanslaus.
Akizungumza kwa tabu na Malunde1 blog ,mwanamme huyo alisema anaitwa
Shaban Charles (30) kutoka kata ya Kitangiri katika manispaa ya Shinyanga
na amefika hapo akitokea kwa mganga wa kienyeji kijiji Mwamala kufuata dawa za
kutafuta mke wake aliyeachana naye na amegoma kurudi nyumbani.
“Nilikwenda kwa mganga baada ya
kuelekezwa kwa mganga huyo akanipa dawa za kuoga na kuchoma akaniambia mke
wangu yupo hapa
Mwenyekiti wa kitongoji cha
Bugayambelele Magharibi Donald Francis alisema alipigiwa simu na kuelezwa
kuwepo kwa mwanamme anayehusishwa na tukio la kubaka wanawake kishirikina na
kuiba simu katika kijiji jirani cha Nhelegani kata ya Kizumbi.
Alisema mwanamme huyo alikutwa na
dawa za kienyeji huku akitoa maelezo yasiyoeleweka ikiwemo kudai amefika hapo
kwa ajili ya kutafuta kazi ya kufyatua matofali,kutafuta mke wake na anatoka
kwa mganga wake wa kienyeji aliyemnyweshwa dawa za ajabu.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa
Shinyanga Elias Mwita alipotafutwa na waandishi wa habari alisema hana muda
kuzungumza na waandishi wa habari mpaka baadaye.
Angalia picha hapa chini
Mwanamme aliyejitambulisha kwa jina la Shaban Charles kutoka Kitangiri katika manispaa ya Shinyanga anayedaiwa kujihusisha na vitendo vya kubaka wanawake kishirikina nyakati za usiku-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Polisi wakiwa eneo la tukio
Wananchi wakiwa eneo la tukio
Dawa za kienyeji alizokutwa nazo jamaa huyo
Dawa za kienyeji za jamaa pamoja simu yake..dawa imeandikwa
“Imala yose -kuchoma kuomba mke wako roho yake ili irudi kwako aje kwako”
Dawa za kienyeji "kuoga na kuchoma kuomba mkeo akupende na arudi kwako”.
Polisi na wananchi wakiwa wamemzunguka jamaa huyo
Mwandishi wa habari wa Radio Faraja Steve Kanyeph akifanya mahojiano na jamaa huyo
Wananchi wakiwa eneo la tukio
Wananchi wakiwa eneo la tukio
Gari la polisi likiwasili eneo la tukio
Jamaa akipanda kwenye gari la polisi
Baiskeli ya mtuhumiwa ikipandishwa kwenye gari la polisi
Polisi wakiondoka na mtuhumiwa
Wananchi wakiondoka eneo la tukio
Mwenyekiti wa kitongoji cha Bugayambelele Donald Francis akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema alipigiwa simu na kuelezwa kuwepo kwa mwanamme anayehusishwa na tukio la kubaka wanawake kishirikina katika kijiji jirani cha Nhelegani kata ya Kizumbi.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
SOMA <<HAPA >>HABARI KUHUSU WANAWAKE KUBAKWA KICHAWI SHINYANGA