
Hii ndiyo hali halisi na changamoto katika sekta ya elimu nchini-Pichani Darasa la awali katika shule ya msingi Sima b katika halmashauri ya mji wa Bariadi mkoa wa Simiyu likiendelea

Darasa linaendelea
SERIKALI imelaumiwa kwa kushindwa kuwekeza rasilimali za kutosha katika
utoaji wa Elimu ya Awali kama inavyoelekezwa na Mtaala wa utoaji wa elimu hiyo
hapa nchini.
Hayo yamebainishwa juzi na Wadau wa Elimu mjini Bariadi wakati wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi katika maeneo tofauti juu ya changamoto
zinazoikabili sekta ya elimu hasa utoaji wa Elimu ya awali.
Walisema kuwa licha ya jamii kuwa na ufahamu wa elimu hiyo lakini
Serikali bado haijawa na nia ya dhati kwa kuelekeza raslimali za kutosha za
kuwezesha kutolewa kwa kiwango kinachokubaliwa kama ilivyoelekezwa na Mtaala wa
Elimu ya awali.
“Jamii kwa sasa imekuwa na
uelewa mkubwa sana juu ya Elimu ya awali ndiyo maana ukitembelea madarasa hayo
yana wanafunzi wengi kuliko uwezo wake lakini jambo la kusikitisha serikali
bado haijaona umuhimu wa kuwekeza ndiyo maana elimu hii katika mazingira yaliyo
mengi ni ya kusikitisha”Alisema Rose John.
Walisema kuwa utoaji wa elimu hiyo wilayani humo umekuwa ukikabiliwa
na changamoto nyingi ambazo ni pamoja ukosefu wa vyumba vya madarasa ya kusomea
wanafunzi huku wengine wakisomea chini ya mti na hata shule zenye madarasa
hayana mahitaji muhimu kwa ajili wanafunzi hao.
Naye Mwalimu, Yunice Mahega anayefundisha darasa la awali katika shule
ya Msingi Sima ‘A’ mjini humo anasema kuwa wana darasa moja la elimu ya Awali
lakini mazingira yake si rafiki kwani kimsingi elimu hiyo inatakiwa kutolewa
katika mazingira maalum tofauti na ilivyo kwa vyumba vya shule za kawaida.
“Chumba cha kufundishia elimu ya Awali kinapaswa kuwa tofauti na
vyumba hivi vingine ona hapa kwetu hiki chumba kinapaswa kutumiwa na wanafunzi
wakubwa na si hawa watoto pia yanapaswa kuwa na madawati ambayo ni mafupi ili
yakidhi vimo vya wanafunzi lakini siye unaona hatuna hata dawati moja watoto
wanakaa chini”,anasema Mwalimu Mahega kwa uchungu.
Aliongeza a kuwa licha ya
kufuata Mtaala katika kufundishia elimu hiyo lakini idadi kubwa ya wanafunzi
darasani ni mojawapo ya tatizo kwani Mtaala unaelekeza uwiano ni chumba kimoja
kwa wanafunzi 25 wakati katika shule hiyo kuna wanafunzi 90.
Akizungumzia hali hiyo Ofisa Elimu Shule za Msingi wa Mji wa
Bariadi,Samwel Muyemba anakiri kuwepo kwa hali hiyo huku akisisitiza ya kuwa
idara yake inajitahidi kukabiliana na changamoto hizo kadri wanavyopata pesa
kutoka serikalini.
Alisema kuwa miundo mbinu si rafiki kuwezesha elimu hiyo kutolewa
kulingana na inavyoelekezwa na Mtaala huku akitolea mfano kuwa shule zilizo
nyingi katika halmashauri hiyo hazina vifaa kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia
na kufundishia pamoja na michezo.
Na Samwel Mwanga-Simiyu
TAFADHALI BOFYA HAPA U LIKE PAGE YETU TUKUTUMIE "HABARI" MOJA KWA MOJA KILA ZINAPOTOKEA
Social Plugin