
Vijana 85 kutoka halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma wamepatiwa mafunzo ya uwekezaji na ufugaji wa kisasa kupitia Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi, inayoratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Songea, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Afisa Uvuvi wa Mkoa, Bw. Basil Amuli, amewataka vijana kutumia kikamilifu mafunzo na mikopo watakayopata kwa kuanzisha na kuendesha miradi yenye tija itakayowawezesha kujiongezea kipato na kujiajiri.
" Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi, hivyo ni wajibu wa wanufaika kuhakikisha wanatumia fursa hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kupata matokeo chanya na kuwa mfano kwa vijana wengine." amesema Bw. Amuli
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo ya Wanufaika Kanda ya Kusini, Dkt. Justinian Lutatina, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea vijana uwezo wa kutumia kwa ufanisi mikopo watakayopata kupitia Programu ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi.
Vilevile ameeleza kuwa vijana hao wanapatiwa mafunzo kuhusu usimamizi wa fedha na mapato, uanzishaji na uendeshaji wa miradi yenye tija pamoja na mbinu bora za ufugaji wa kisasa wa nguruwe, mbuzi na kuku ili kuwawezesha kuendesha miradi yenye tija na endelevu.
Baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo hayo wamesema mafunzo yamewapa maarifa mapya kuhusu ufugaji wa kisasa, usimamizi wa miradi na matumizi sahihi ya mikopo, huku wakieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato chao.
Vijana hao pia wametoa wito kwa wenzao kujitokeza kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia mafunzo na mikopo ya uwezeshaji kiuchumi ili kujenga maisha bora na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Social Plugin