
Viongozi wa halmashauri nchini wamekumbushwa kuanza maandalizi ya kuweka miundombinu wezeshi kukudhi mahitaji kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028 ambapo madarasa ya saba na la sita watahitimu kwa pamoja.
Aidha, imesisitizwa kuwa maandalizi hayo yahusishe ujenzi wa madarasa, mabweni na miundombinu mingine muhimu ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata nafasi ya kuendelea na masomo bila changamoto.
Wito huo umetolewa wilayani Kilwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, Agosti 3,2026 alipokuwa akizindua mabweni mawili katika Shule ya Sekondari Mtangani yaliyogharimu zaidi ya shilingi milioni 362.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kwa kuwa ndiyo msingi wa ukombozi wa wananchi na maendeleo ya haraka ya Taifa.
Amefafanua kuwa, katika Wilaya hiyo, Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.477 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu ya sekondari, hatua ambayo imeleta mageuzi makubwa katika miundombinu ya elimu na kuongeza fursa za wanafunzi kusoma katika mazingira salama na rafiki.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilwa Kusini Hasnain Dewji amesema kuwa kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa, hivyo amewahakikishia wananchi wa Kilwa kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha sekta hiyo muhimu.


Social Plugin