
Na Oscar Assenga, TANGA
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Tanga Rashid Mchatta amefungua kikao kazi cha Wakurugenzi na Mameneja wa Huduma kwa Wateja wa Mamlaka za Maji nchini huku akisisitiza matumizi teknolojia ya kisasa katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao.
Wito huo umetolewa jijini Tanga na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, wakati akifungua kikao kazi cha Wakurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Sekta ya Maji nchini.
Kikao hicho kinafanyika chini ya kaulimbiu “Huduma Janja: Matumizi ya Teknolojia kwa Huduma Bora kwa Wateja”, kikilenga kuwawezesha wakurugenzi na mameneja hao kubadilishana uzoefu na kujadili mbinu mbalimbali za kuboresha huduma kwa wananchi.
Mchatta aliipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiamini na kuiwezesha Wizara ya Maji kutekeleza miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na huduma za usafi wa mazingira nchini.
Pia aliipongeza uongozi wa Wizara ya Maji unaoongozwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Naibu Waziri, Mhandisi Mathew Kundo, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, Rose Ambrose, kwa juhudi wanazofanya katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.
Alisema mafanikio yanayoonekana katika sekta ya maji, kuanzia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati hadi uboreshaji wa huduma kwa wananchi, yanaonesha kuwa uongozi wa wizara hiyo umejikita katika kuhakikisha huduma zinaboreshwa kila siku.
“Viongozi hawa wameonesha weledi, uzoefu na uthubutu katika kusimamia sekta ya maji. Ushirikiano wao umeendelea kuleta mafanikio yanayoonekana na wananchi wanaendelea kushuhudia mabadiliko katika huduma za maji na usafi wa mazingira,” alisema Mchatta.
Alisema kikao hicho ni fursa muhimu kwa wakurugenzi na mameneja wa huduma kwa wateja kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza katika utoaji wa huduma.
Kwa mujibu wa Mchatta, mafunzo hayo pia yanahusu ufanisi wa biashara katika mamlaka za maji pamoja na mbinu za uwekezaji binafsi, ambapo wataalamu kutoka UTT-AMIS wanashiriki kutoa elimu kwa washiriki.
Aliwataka washiriki kutumia kikamilifu fursa hiyo kujifunza mbinu mpya, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazowakabili katika utoaji wa huduma kwa wateja.
“Ninaamini mafunzo haya yatakuwa chachu ya kuboresha ufanisi mtakaporudi katika vituo vyenu vya kazi na hivyo kuongeza ubora wa huduma mnazozitoa kwa wananchi,” alisema.
JUKWAA LA WAKURUGENZI LAZIDI KUKUA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mamlaka za Maji nchini, Alawi Ahmad, alisema jukwaa hilo ni sehemu muhimu ya uongozi katika sekta ya maji, kwa kuwa linawapa nafasi wakurugenzi na mameneja kukutana, kujadiliana na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili katika utoaji wa huduma.
Alisema jukwaa hilo limekuwa likifanya vikao kila mwaka na kwa sasa lina takribani miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
“Jukwaa hili limekuwa likitusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utoaji wa huduma kwa wateja na pia limetumika kama sauti ya pamoja ya wakurugenzi wa huduma kwa wateja katika sekta ya maji,” alisema Ahmad.
Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Abbas Muslim Pyarali alisema kikao hicho kinawakutanisha wakurugenzi wa mamlaka za maji wanaojikita katika utoaji wa huduma kwa wateja.
Abbas ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Maji alisema kikao hicho kitakachodumu kwa siku tatu kitawapa washiriki nafasi ya kupata mafunzo maalumu na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Maji za kuhakikisha huduma za maji safi na usafi wa mazingira zinaendelea kuboreshwa nchini.
Social Plugin