
Na Bora Mustafa, Arusha
Mdau wa michezo, Champion D, ametembelea Kituo cha Watoto Yatima cha Paradiso Mpya kilichopo Kata ya Sinoni, mkoani Arusha, na kukabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Akizungumza Agosti 3, 2026, baada ya kukabidhi msaada huo, Champion D amesema wazo la kuanzisha shughuli hiyo lilianza zaidi ya miaka mitatu iliyopita baada ya kuona watu kutoka maeneo mbalimbali nchini wakifanya matendo ya kusaidia jamii.
Amesema safari ya kufanikisha wazo hilo haikuwa rahisi kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kupata wadau na kufanya maandalizi, lakini hakukata tamaa kwa kuwa aliamini dhamira yake ya kusaidia jamii ilikuwa muhimu.
Aidha, amewashukuru wadau wote waliomuunga mkono, wakiwemo watu kutoka sekta ya michezo, marafiki pamoja na mke wake, ambaye amesema amekuwa nguzo muhimu katika kufanikisha shughuli hiyo.
Kwa upande wake, mmoja wa walezi wa Kituo cha Paradiso, Mama Kaaya, amesema kituo hicho kilianza na watoto wanane, lakini kwa sasa kinahudumia watoto 27.
Ameeleza kuwa licha ya kutokuwa na biashara wala chanzo rasmi cha mapato, wameendelea kuwahudumia watoto hao kwa neema ya Mungu na misaada kutoka kwa wasamaria wema.
Aidha, amesema watoto wengi waliokulia katika kituo hicho wamehitimu masomo yao, wengine wamepata ajira, na bado wanaendelea kurejea kukitembelea kituo hicho.
Mama Kaaya pia ametoa shukrani kwa Champion D na wadau wake kwa msaada walioutoa, akisema umefika wakati ambao kituo kilikuwa kinapitia kipindi kigumu.
Naye Riziki Yusuf Bendera amesema kitendo kilichofanywa na Champion D kinapaswa kuwa mfano kwa vijana wengine pamoja na watu wote wanaofanya kazi katika sekta ya michezo na vyombo vya habari. Amesema kutoa sehemu ya walichonacho kwa jamii ni ishara ya uwajibikaji, mshikamano na upendo.
Kwa upande wake, Mary Yohanes, mwanafunzi wa kidato cha pili, ametoa shukrani kwa wote waliochangia msaada huo. Amesema kituo hicho bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo upatikanaji wa chakula, mavazi na ada za shule kwa baadhi ya watoto. Aidha, amewaombea wote waliowasaidia Mungu awabariki na awaongezee uwezo wa kuendelea kuwasaidia wenye uhitaji.
Social Plugin