Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AFDB: UBIA WA SEKTA YA UMMA NA BINAFSI WAINUA MINYORORO YA THAMANI YA KILIMO



Na Sheila Ahmadi, Dodoma

Taasisi ya Kuendeleza Shoroba za Kilimo Tanzania (TAF/AFORD) imesema ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo umeendelea kuwa kichocheo muhimu katika kuongeza tija, uzalishaji na thamani ya mazao ya kilimo nchini.

Akizungumza katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Nane Nane, Dodoma, Meneja wa Masuala ya Ushirikiano na Ubia wa Kikundi cha Thamani, Khalid MGaramo, amesema taasisi hiyo inafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali, sekta binafsi pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuboresha minyororo ya thamani ya mazao.

MGaramo amesema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha changamoto zinazowakabili wadau katika uzalishaji, masoko, mazingira ya biashara, teknolojia na uwekezaji zinapatiwa suluhisho kwa pamoja.

Amesema taasisi hiyo imejikita zaidi katika Shoroba ya Kusini inayohusisha mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma, huku ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kuibua fursa na kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye minyororo ya thamani.

“Tunashirikiana na sekta ya umma, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo kwa lengo la kuleta mabadiliko katika kilimo cha Tanzania na kuboresha maisha ya wakulima,” amesema MGaramo.

Ameongeza kuwa katika utekelezaji wa shughuli hizo, taasisi hiyo hushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na wizara na taasisi nyingine zinazogusa sekta ya kilimo, ikiwemo mifugo na uvuvi, ardhi na mazingira.

MGaramo amesema moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele ni kuongeza tija kwa wakulima, ambapo uzalishaji mdogo ni miongoni mwa sababu zinazofanya baadhi ya wakulima kushindwa kupata bei nzuri katika masoko.

Amesema kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia bora, pembejeo sahihi na kuboresha afya ya udongo ni muhimu ili mkulima aweze kuzalisha kwa kiwango kinachomwezesha kushindana katika soko.

“Changamoto ya bei mara nyingi inatokana na uzalishaji mdogo. Kama mkulima anazalisha magunia mawili kwa ekari wakati mwingine, na mwingine anazalisha magunia 10, gharama za uzalishaji zinaweza kuwa zinafanana, lakini mwenye uzalishaji mkubwa anakuwa na uwezo wa kushindana zaidi sokoni,” amesema.

MGaramo ameongeza kuwa taasisi hiyo inahamasisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ili Tanzania isiendelee kuuza mazao ghafi na kupoteza fursa za ajira na mapato zinazoweza kupatikana katika hatua za kuongeza thamani.

Ametoa mfano wa zao la parachichi, ambalo linaweza kutumika kuzalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo mafuta, hivyo kuongeza thamani ya zao hilo na kutoa fursa zaidi kwa wakulima na wawekezaji.

Vilevile, hatua hiyo inasaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi, wakati malighafi zinazohitajika kuzalisha bidhaa hizo zinapatikana nchini.

Katika mazao mengine, MGaramo amesema wameendelea kuhamasisha uzalishaji wa mazao yenye soko la uhakika, ikiwemo viazi, pamoja na kuimarisha usindikaji wa mazao kama mpunga ili bidhaa zinazozalishwa ziweze kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema changamoto mbalimbali za kimataifa, ikiwemo athari za UVIKO-19, migogoro ya kimataifa na changamoto za usafirishaji, zimeongeza umuhimu wa Tanzania kuimarisha uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ndani ya nchi.

MGaramo amesema Maonesho ya Nane Nane ni fursa muhimu ya kuwaunganisha wakulima na wadau wa mnyororo mzima wa thamani, wakiwemo wazalishaji wa pembejeo, teknolojia, taasisi za kifedha, wasindikaji na wanunuzi.

Kupitia ushirikiano huo, lengo ni kujenga mfumo wa kilimo jumuishi ambao unamnufaisha mkulima mdogo, mwekezaji na wadau wengine wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani.

“Tunataka uwekezaji unaofanyika kwenye kilimo uzingatie wakulima wanaozunguka maeneo hayo, kwa kuwapatia soko, teknolojia na bei shindani, ili maendeleo yatakayopatikana yawe jumuishi,” amesema.

Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, baadhi ya wakulima ambao awali walikuwa wakitegemea msaada wameanza kujenga uwezo wa kuzalisha na kufanya shughuli zao kwa tija zaidi, hatua inayosaidia kuboresha maisha yao na kuchochea maendeleo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com